Ezekiel Mutua amtunuku Mulamwah Sh20,000 baada ya kumaliza mzozo wao wa mwaka mmoja

Muhtasari

•Wawili hao walikutana katika hafla iliyofanyika Jumatatu na kushiriki mazungumzo ambayo yalipelekea kusuluhishwa kwa ugomvi wao.

•Februari mwaka jana Mulamwah alimkashifu bosi huyo wa MCSK hadharani kwa kutotimiza ahadi ya kuunga mkono sanaa yake.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Hatimaye mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah na Mkurugenzi Mtendaji wa MCSK Ezekiel Mutua wamezika ugomvi wao katika kaburi la sahau.

Wawili hao ambao wamekuwa wakizozana kwa zaidi ya mwaka mmoja walikutana katika hafla iliyofanyika Jumatatu na kushiriki mazungumzo ambayo yalipelekea kusuluhishwa kwa ugomvi wao.

Mulamwah alisema kuwa yeye na Mutua sasa ni marafiki wakubwa na kutangaza kuwa anatazamia kufanya kazi pamoja naye katika siku za usoni.

"Jana tulikutana na Dkt Ezekiel Mutua, tukazungumza na kuweka tofauti zetu kando. Sisi sasa ni marafiki wakubwa. Ugomvi umezikwa. Tunatazamia kufanya kazi na MCSK katika siku za usoni kama ilivyoahidiwa. Asante kaka," Mulamwah alitangaza Jumanne kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mchekeshaji huyo ambaye pia ni muuguzi alifichua kuwa Dkt. Mutua alimtumia Ksh20,000 baada ya ugomvi wao kufika hatima.

Februari mwaka jana Mulamwah alimkashifu bosi huyo wa MCSK hadharani kwa kutotimiza ahadi ya kuunga mkono sanaa yake.

"Habari bwana Ezekiel Mutua, ni karibu mwaka sasa tangu ahadi yako, ulimaanisha au ulikuwa unaandika tu kwa wakati huo, au mimi "sipatikani"? Ikiwa serikali haiwezi kutusaidia kama vijana, basi tafadhali usiweke matumaini ya uongo ndani yetu, ni bora utuache tuteseke kwa amani," Mulamwah alimwambia Mutua kupitia Twitter.

Takriban miaka miwili iliyopita Dkt Mutua ambaye kwa wakati huo alikuwa bosi wa KFCB aliahidi kumsaidia Mulamwah kufufua sanaa yake baada ya kutangaza kuwa yupo tayari kuacha uchekeshaji.

Mchekeshaji huyo alitishia kuacha ucheshi akilalamika kuwa unyanyasaji wa mitandaoni ulikuwa umemsababishia msongo wa mawazo.

"Ninasikia kwamba watumizi wa Twitter wanamfukuza Mulamwah kutoka kwenye uchekeshaji na kuingia kwenye mafadhaiko. Kaka jiinue na unipigie simu. Nitakununulia shati jipya, nitakushauri na kukufanya kuwa balozi wa sanaa safi. Njia bora ya kukabiliana na wanyanyasaji wa mtandao ni kukataa kukata tamaa," Mutua alimwambia Mulamwah kupitia Twitter.

Kulingana na Mulamwah, bosi huyo wa MCSK hakuwa ametimiza ahadi hizo zake mwaka mmoja baadae.