"Njia zetu zitakutana tena" Omosh amuaga marehemu baba yake kwa hisia kemkem

Muhtasari

•Mzee David Kamau ambaye aliaga dunia mapema mwezi huu alizikwa nyumbani kwake siku ya Jumatano.

Image: INSTAGRAM// OMOSH KIZANGILA

Muigizaji wa Tahidi High Joseph Kinuthia almaarufu Omosh hatimaye amempungia mkono wa buriani marehemu baba yake.

Mzee David Kamau ambaye aliaga dunia mapema mwezi huu alizikwa nyumbani kwake siku ya Jumatano.

Omosh alitumia ukurasa wake wa Instagram kumuaga baba yake huku akieleza matumaini yake ya kumuona tena.

"Imekuwa safari ndefu lakini njia zetu zitakutana tena. Pumzika kwa amani baba," Omosh aliandika Jumatano.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha yake akiwa amesimama mbele ya kaburi la marehemu baba yake.

Image: INSTAGRAM// OMOSH KIZANGILA

Muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 52 alitangaza habari kuhusu kifo cha baba yake mnamo Juni 5. Katika tangazo lake, Omosh alisema kuwa marehemu atakumbukwa milele na daima. 

"Utakumbukwa milele na milele. Matukio mazuri uliyoshiriki nasi daima yatazungumza juu ya mtu bora ambaye ulikuwa. Pumzika kwa amani Baba," Omosh alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mchekeshaji huyo aliambatanisha ujumbe huo na picha inayoonyesha akiwa amemshika mzazi huyo wake kwenye bega.

Mzee Kamau pia ndiye baba wa muigizaji mkongwe Naomi Kamau ambaye aliigiza kama mama ya Tina na Mike katika kipindi cha Mother-in-Law.