Eric Omondi asimulia jinsi ex wake Chantal alivyoshambuliwa na mpenzi wake wa sasa

Muhtasari

•Eric alilaani vikali shambulio hilo dhidi ya mpenzi wake wa zamani na kutishia kuchukua hatua ya kisheria dhidi ya Traldi.

•Mchekeshaji huyo alidai kuwa Traldi amekuwa akimshambulia kipusa huyo mwenye asili ya Italia kwa muda mrefu.

Nicola, Chantal na Eric Omondi
Nicola, Chantal na Eric Omondi
Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji Eric Omondi ameripoti mchumba wa sasa wa aliyekuwa mpenzi wake Chantal Grazioli kwa madai ya dhuluma.

Adhuhuri ya Ijumaa mchekeshaji huyo aliibua madai kuwa Bw Nicola Traldi alimshambulia Chantal na kumsababishia majeraha mwilini.

Eric alilaani vikali shambulio hilo dhidi ya mpenzi wake wa zamani na kutishia kuchukua hatua ya kisheria dhidi ya Traldi.

"Mwanaume yeyote anayewekelekea mikono yake kwa mwanamke ni MUOGA!!! Nicola Traldi ni Muoga. Ni Dhaifu na Hajiamini. Nguvu za mwanaume huonyeshwa kikamilifu anapomlinda mwanamke na sio anampiga," Eric alisema.

Kwenye Instastori zake, mchekeshaji huyo alionyesha ripoti ya uchunguzi wa kimatibabu ambayo iliashiria kuwa mguu wa Chantal umevunjika.

Eric akiwa kwenye mahojiano alifichua kuwa mpenzi huyo wake wa zamani aliweza kupokea matibabu. Pia alidai kuwa polisi wameanzisha msako dhidi ya Traldi.

"Kama mimi ningekuwa yeye ningeenda tu mwenyewe kwa polisi. Asingoje kuendewa," Eric alisema.

Mchekeshaji huyo alidai kuwa Traldi amekuwa akimshambulia kipusa huyo mwenye asili ya Italia kwa muda mrefu.

Alidai kuwa Chantal alimpigia simu mwendo wa saa mbili asubuhi ya Ijumaa kumwarifu jinsi mpenzi wake alivyomshambulia.

"Nilipata Chantal amevunjika mguu. Alikuwa amenyongwa kwa shingo. Alikuwa ameangushwa kwa ngazi. Vitu vilikuwa vimepasuka. Ni mlinzi, majirani na caretaker ambao walimsaidia," Alidai Eric.

Mchekeshaji  huyo alitumia fursa hiyo kuwashauri wanadada kugura ndoa au mahusiano pindi yanapoanza kuwa sumu.

Bw Traldi hata hivyo tayari amejitokeza kutupilia mbali madai ya kumdhulumu mpenziwe yaliyoibuliwa na Eric.

Huku akijitetea, Traldi alisema madai ya Eric si ya kweli huku akidai kuwa hana uwezo wa kupiga mwanamke. 

"Nimesingiziwa kwa jambo ambalo singefanya kamwe, lisilosemeka, Ni siku ya huzuni.. Nisingewekelea mikono yangu juu ya mwanamke. Mimi ni baba wa mabinti wawili. Ukweli utajulikana," Aliandika.

Mjasiriamali huyo alibainisha kuwa mama yake alimfunza maadili mema na hata watu wa karibu naye wanafahamu hawezi kupiga mwanamke.