{Video} "Sitaki kufa tafadhali!" mtoto anayeugua kansa alilia msaada

Mtoto huyo alisema amewakosa wanafamilia wake kutokana na kulazwa juu ya saratani. Aliwataka wasamaria wema kujitokeza na kumsaidia gharama ya matibabu.

Muhtasari

• "Ninaogopa kwamba huenda sitarudi nyumbani na sitaona familia yangu tena" mtoto huyo alilia huku akiomba msaada wa matibabu.

Jumatano video moja ya kutia huruma ya mtoto mmoja mdogo kutokea Nigeria akilia baada ya kutambuliwa kuwa na ugonjwa wa saratani imesambazwa sana huku wengi wakimhurumia mtoto huyo ambaye alikuwa analia akisema kwamba hataki kufa.

Taarifa iliyoambatanishwa na video hiyo ni kwamba daktari waliambia wazazi wake kuwa ugonjwa huo wa kansa unazidi kusambaa mwilini mwake kwa kasi ya ajabu na anahitaji kutibiwa haraka iwezekanavyo.

Mtoto huyo aliyetambuliwa kwa jina la Alexandra alionekana akilia huku akiwaomba wahisani wema kumsaidia kifedha ili kutibiwa kwani hayuko tayari kufa.

Katika video hiyo ya kutia huruma, mtoto Alexandra anasikika akisema kwamba amewapeza sana wazazi wake na ndugu zake nyumbani na anataka kusaidiwa kwa matibabu ili aweze kurudi na kujumuika na familia yake.

“Sitaki kufa tafadhali. Jina langu ni Alexandra na nina saratani. Ninaogopa kwamba huenda sitarudi nyumbani na sitaona familia yangu tena. Ninamkumbuka mama yangu na dada yangu. Sitaki kufa na kuwaacha. Matibabu yangu yanagharimu pesa nyingi na wazazi wangu hawana pesa za aina hiyo. Tafadhali nisaidie nipone. Tafadhali. Sitaki kufa,” mtoto Alexandra anaonekana akilia kwa huruma.

Katika video hiyo, anaonekana mwanaume mmoja anayekisiwa kuwa babake akimfariji baina ya kwikwi za kilio kichungu huku akimuahidi kwamba familiqa inampenda na kumpa tumaini la kupona.

“Usihofu, utakuwa sawa, sawa?” mwanaume huyo anamfariji huku akimpapasa kwa upendo mkubwa mtoto Alexandra.

Video hiyo iligusa nyoyo za watu wengi mitandaoni ambapo wengi walifurika kumtakia kila la kheri na kumpa tumaini kwamba kwa kuwa tayari ashalisema kutoka moyoni kwamba hataki kufa, basi litatimia na hawezi kufa bali atapata msaada, atatibiwa na kurudi kujumuika na familia yake ambayo ugonjwa wa saratani umemtenganisha nayo kwa muda mrefu sasa.

Mtoto huyo alielezea kwamba familia yake ni ya maisha yenye uchumi wa kadri ambao hawana uwezo wa kukimu kiasi kikubwa cha gharama ya matibabu kinachohitajika hospitalini na hivyo kuwaomba watu kusaidia familia yake kupata japo hela ya matibabu kwa kuwa daktari alishatoa tahadhari kwamba kansa tayari imesambaa mwilini mwake pakubwa.