"Wanaume wote wanapenda wake wengi, tia bidii uwe chaguo la kwanza" Letoo awashauri wanawake

Letoo aliachana na mkewe mwaka 2021 na kwa sasa wanashirikiana kulea mwanao mmoja wa kiume

Muhtasari

• “Tamaduni za Kiafrika zinaruhusu mwanaume mmoja kuoa wanawake wengi, jamani tukumbatie tamaduni hiyo,” - Letoo.

Mwanahabari Stephen Letoo na mwanawe
Image: Stephen Letoo (Facebook)

Mwanahabari Stephen Letoo amezua mjadala mkali mitandaoni baada ya kudai kwamba wanaume wote pasi na kubagua kipato, rangi au kabila ni wenye wake wengi.

Akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumatano, Letoo alisema kwamba wanaume wote kawaida yao ni kuwa na wanawake au wapenzi wengi na kuwashauri wanawake kutia bidi ili kuwa chaguo la kwanza kwa sababu ukweli utabaki pale pale kwamba huyo mwanaume atakuwa na wanawake wengine.

Kulingana na Letoo, kila mwanaume ana wanawake zaidi ya mmoja na yule anayefikiria kwamba mumewe anampenda peke yake basi ana bahati kwa sababu alitia bidi na kuchukua nambari ya kwanza, ila ajue fika kwanza foleni ni ndefu nyuma yake.

“Wanaume wote ni wenye wanawake wengi, wewe kama mwanamke, ni lazima utie bidii ili kuwa chaguo la kwanza.” Aliandika Letoo.

Ripota huyo wa runinga moja nchini alidokeza kwanza alikuwa katika kaunti ya Nyamira ambako pia alisema kwamba Kaunti hiyo ina wanawake warembo wengi.

Miaka miwili iliyopita, Letoo na aliyekuwa mke wake Winnie Nadupoi walitengana na kila mmoja kuenda zake.

Katika mahojiano na wakuza maudhui kipindi hicho, Letoo alifichua kwamba walisha achana na kilichobakia ni kushirikiana kulea mwanao wa kiume na pia kusema kwamba yeye siku zote ana fikra za kuwa mwanaume mwenye wanawake wengi kwa sababu baba yake na babu yake walikuwa na wake zaidi ya mmoja ambapo alisema kwamba katika jamii yake ya Kimasaai, kuwa na wanawake wengi ni jambo la kusherehekewa.

Hii si mara ya kwanza Letoo anasisitizia suala la mwanaume kuwa na wanawake wengi ambapo wengi wanakisia ndicho chanzo kikubwa kilichosambaratisha mahusiano yake na Nadupoi kwani inaeleweka kwamba wanawake wengi wamezaliwa na wivu na si rahisi kukubali kuolewa mke mwenza.

“Tamaduni za Kiafrika zinaruhusu mwanaume mmoja kuoa wanawake wengi, jamani tukumbatie tamaduni hiyo,” Letoo aliwahi andika kwenye Facebook yake.

Baadhi wanakubaliana naye huku wengine wakitofautiana kwa kusema kwamba maisha ya sasa ni magumu mno na mwanaume kuwa na wanawake zaidi ya mmoja ni kibarua kigumu sawa sawa na kukwea mchongoma.