Kinuthia ampasha mtangazaji kwa kumuuliza kama yeye ni shoga

Kwa kuchukizwa, Kinuthia alimwambia maswali kama hayo hayana umuhimu kabla ya kukata simu.

Muhtasari

• Kinuthia aliletana juu na mtangazaji aliyetaka kubaini mrengo wake wa kingono na kusema kwamba maswali kama hayo hayafai.

Mkuza maudhui Kelvin Kinuthia
Image: OfficialKinuthia (Instagram)

Mkuza maudhui kwenye mtandao wa TikTok, Kelvin Kinuthia alichukizwa na kitendo cha mtangazaji mmoja kumuuliza iwapo yeye ni wa mrengo ule mwingine kingono ama yupo katika njia kuu kama mtu wa kawaida.

Swali hilo lilimchukiza Kinuthia ambapo alikataa katakata kulijibu huku akisisitiza kwamba maswali ya sampuli hiyo si ya maana kabla ya kukata simu.

“Kuna kitu hapa kidogo kinatuchanganya kulingana na maudhui yako Kinuthia, vipi uko sawasawa kweli kwamba wewe ni mtu unapenda wanadada ama kidogo umepinda Kinuthia?” Aliuliza mtangazaji huyo aliyempigia simu mkuza maudhui Kinuthia.

Ni kama swali hili lilimpata Kinuthia pasi na kujitayarisha na alikata simu ghafla, kitendo kilichoonesha kwamba swali hilo halikumuingia kabisa na hakuwa tayari kulijibu. Mtangazaji alimpigia simu kwa mara ya pili na hapo ndipo Kinuthia alitema moto na kumpasha makali yake mubashara.

“Ni nini, maswali kama hayo yanatoka wapi? Haina umuhimu kabisa, halafu mbona unanipigia simu kuniuliza maswali kama hayo? Maswali kama hayo hayana tija yoyote na si muhimu, ahsante,” alisema Kinuthia na kukata simu tena kwa ghadhabu kubwa.

Ikumbukwe Kinuthia amekuwa akigonga vichwa vya habari za umbea nchini kutokana na jinsi anavyovaa nguo za kike ambazo zinawiana barabara na mwili wake wa kibongebonge, jambo ambalo limekuwa likizua maswali mengi kuliko majibu kuhusu jinsia halisi ya kijana huyo.

Miezi michache iliyopita katika mahojiano ya kipekee na mkuza maudhui mmoja, Kinuthia alikataa kuzungumzia jinsia yake halisi na kusema kwamba ni wakati sasa watu wakome kumuwekea maneno mdomoni mwake kwamba amesema mambo fulani fulani.

Aliweka wazi kwamba yeye hajawahi kumwambia mtu yeyote kuhusu maisha yake ya kingono na hivyo watu waache kusema kwa niaba yake.

Kinuthia aligoma kutegua kitendawili hicho na kusema kwamba upo muda atakuja kuwaelezea mashabiki wake ukweli wake kuhusu mrengo wake wa kingono.

Juzi kata alionekana kwenye picha wakiwa wamepakatana na mkuza maudhui mwingine almaarufu Mtumba Man ambapo alifuatisha picha hiyo kwa ujumbe wa kimahaba, jambo ambalo pia lilizua mjadala mkali wengine wakihisi huenda ako kile chama cha kupandisha bendera kwa mkono mmoja.

Kwenye utambulisho wake instagram, Kinuthia ameweka kwamba yeye anaweza kuwa aidha mwanaume au mwanamke.