"Ninahisi kukosa hewa nikiwa Kenya!" Akothee alalamika

Muhtasari

•Akothee ameeleza kuwa wakati mwingine huwa anatamani kuwa peke yake bila walinzi au watu wengine waliondamana naye.

•Akothee alieleza jinsi alivyokuwa amepeza uhuru wa kutembea bila usumbufu wowote na hewa safi.

Image: HISANI

Mwanamuziki na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu Akothee ameendelea kulalamikia athari hasi ambazo umaarufu umemletea.

Akothee ambaye kwa sasa yupo katika ziara ya kikazi nchini Ujerumani amebainisha kuwa umaarufu umemnyima nafasi kuwa pekee yake.

Mama huyo wa watoto watano ameeleza kuwa wakati mwingine huwa anatamani kuwa peke yake bila walinzi au watu wengine walioandamana naye..

"Umaarufu umeniondolea nafasi yangu, ninahisi kukosa hewa Kenya, wakati mwingine nataka kutembea hivi huko CBD bila walinzi na watu walioandamana nami , nimechoka kuwa na watu kuwa wamenizunguka," Akothee alisema  kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mwanamuziki huyo aliambatanisha ujumbe wake na video inayomuonyesha akitembea  pekee yake katika jiji la Paris, Ufaransa.

Akothee alieleza jinsi alivyokuwa amepeza uhuru huo wa kutembea bila usumbufu wowote na hewa safi.

"Huna ufahamu jinsi hii inavyohisi," Alisema.

Mwanzilishi huyo wa Akothee Safari's anatarajiwa kutumbuiza jijini Munich  leo (Jumamosi) mwendo wa saa nne usiku.

Hii sio mara ya kwanza ya Akothee kulalamika kuhusu masaibu ambayo yamesababishwa na umaarufu mkubwa aliojizolea.

Takriban wiki mbili zilizopita mwanamuziki huyp alidai kwamba kwa kipindi cha takriban miaka mitano ambacho kimepita hajakuwa na uhuru wa kutembea mitaani. Alieleza kuwa umaarufu wake mkubwa umefanya hata iwe vigumu kwake kuendesha gari jijini Nairobi.

"Wakati ambao bado ningeweza kutembea kwa uhuru katika CBD, Sasa hata huwa siendeshi gari huko. Imekuwa miaka mitano ya kukosa uhuru wangu," Alisema.

Alieleza kuwa sasa imekuwa ngumu kwake kutembea jijini Nairobi kwa kuwa  anayavutia macho ya wengi kutokana na umaarufu wake.

Akothee alijitosa kwenye taaluma ya muziki zaidi ya mwongo mmoja uliopita. Alijizolea umaarufu mkubwa kati ya mwaka wa 2014-2016.

Taaluma ya mwanamuziki huyo ambaye pia ni mfanyibiashara imezingirwa na utata mwingi kutokana na mtindo wake wa maisha.

Inaaminika kuwa yeye ni miongoni mwa wasanii tajiri zaidi nchini Kenya na hata katika ukanda wa Afrika Mashariki.