"Zuuh ni wengi!" Zuchu hatimaye ajibu baada ya Diamond kujitambulisha kama mumewe

Zuchu amepingana na matamshi ya Diamond kuwa ni mume wake.

Muhtasari

•Diamond aliwasisimua wanamitandao kwa kujitambulisha kama 'mume wa Zuuh' kwenye mtandao wa Instagram. 

•Zuchu amedai kuwa hakuona comment hilo la bosi wake na hata kuzua shaka ikiwa kwa kweli ni yeye alitajwa.

Diamond na msanii wake Zuchu ambaye anadaiwa kuwa kwenye mahusiano naye
Diamond na msanii wake Zuchu ambaye anadaiwa kuwa kwenye mahusiano naye
Image: KWA HISANI

Zuchu kwa mara ya kwanza amevunja ukimya na kujibu baada ya bosi wake Diamond Platnumz kujitambulisha hadharani kama mume wake.

Jumapili, Diamond aliwasisimua wanamitandao kwa kujitambulisha kama 'mume wa Zuuh' kwenye Instagram. 

Hilo lilijitokeza kwenye ukurasa rasmi wa WCB ambapo Diamond alikuwa akicomment  kuhusu video iliyomuonyesha akitumbuiza mashabiki wake nchini Ureno.

"ALIZALIWA ILI KUBURUDIKISHA DUNIA 🌍🌎🌎 PICHA YA KARIBU YA SIMBA 🦁 MFALME MR ELECTRICITY JUKWAANI 🙌🙌🙌. Matumbuizo ya  @diamondplatnumz Moja kwa moja Katika @afronation huko Ureno," Maelezo ya WCB chini ya video hiyo yalisoma.

Katika video hiyo Diamond alionekana akifanya sarakasi mbalimbali jukwaani huku wimbo wake 'Number One' ukicheza.

Yeye ni miongoni mwa mamia ya wanamitandao waliochukua hatua ya kutoa maoni kuhusiana na video hiyo.

"Huyo ni mume wa Zuuh," Aliandika.

Hatua hii ilichukuliwa kama thibitisho lake kuwa kwa kweli yuko kwenye mahusiano ya kimapenzi na Zuchu.

Akizungumza na mtangazaji wa Wasafi Media Ankali Mambi kwa njia ya  simu siku ya Jumanne, Malkia huyo wa Bongo hata hivyo alionekana kupingana na maoni ya wengi.

Zuchu alidai kuwa hakuona comment hilo la bosi wake na hata kuzua shaka ikiwa kwa kweli ni yeye alitajwa.

"Zuuh wako wengi. Ni kweli naitwa Zuuh lakini si Zuuh mimi, kama ingekuwa mimi angeniambia. Itakuwa Zuuh mwingine," Zuchu alisema.

Zuuh ni jina la utani la staa huyo kutoka Zanzibar.

Jibu hilo lake linaonekana kuibua utata mpya kuhusu uhusiano wake halisi na Diamond  ambaye kwa kipindi kirefu hasa mwaka huu imedaiwa kuwa mpenzi wake.

Wawili hao hata hivyo hawajawahi kujitokeza hadharani kukirikuwa wanachumbiana. Hapo awali waliwahi kukana madai ya mahusiano huku Zuchu akiweka wazi kuwa Diamond ni bosi wake tu.

Katika mahojiano yake na Ankali, binti huyo wa Khadija Kopa bado alisistiza kuwa  uhusiano wake na Diamond ni wa kikazi.