Mtoto shujaa: Kijana wa miaka 6 awaokoa wapwa zake kutoka motoni

Richard Kitonga aliwaokoa wapwa zake wa miaka 4 na 2 mtawalia kutoka nyumba iliyokuwa inachomeka.

Muhtasari

• Majirani waliguswa na kitendo hicho cha ushujaa na kuamua kuchangisha kuikarabati nyumba ile.

Kijana Richard pamoja na wapwa zake aliowaokoa kutoka kwa moto
Kijana Richard pamoja na wapwa zake aliowaokoa kutoka kwa moto
Image: YouTube (Screenshot)

Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 6 kutoka kaunti ya Machakos amemiminiwa sifa kama shujaa na watu mitandaoni baada ya habari zake kuibuka kwamba alifanikiwa kuwaokoa wapwa zake wawili wachanga kutoka jumba lililokuwa linaungua.

Hadithi hiyo ya kukosha nyoyo za wengi iliangaziwa katika runinga moja ya humu nchini ambayo ilielezea kwamab kijana huyo kwa jina Richard Kitonga mwenye umri wa miaka 6 tu alifanikiwa kuwaokoa wapwa zake wawili Panda na Christine wenye umri wa miaka 4 na miwili mtawalia kutoka nyumba iliyokuwa ikichomeka.

Inaarifiwa moto ulizuka katika nyumba ambayo watoto hao walikuwa pasi na uwepo wa maam yao na moto ulianza Kitonga aliwatoa watoto hao wenzake karibu na moto na kuwasogeza katika sehemu moja ambayo kulingana na mawazo yako madogo ilionekana kuwa salama kabla ya kuwatoa nje na kuitisha usaidizi wa majirani kuuzima moto ule.

Kitonga aliachwa katika uangalizi wa wapwa zake waakti mamake alienda katika ibada ya kanisa ambapo alitoka na Richard kumnunulia pipi na kumuamuru arudi ili aangalie wapwa zake.

Majirani walisema walipofika walipata sehemu ya sebuleni imeshika moto mkubwa ambao ulichoma vitu kadhaa vya mama huyo mjane.

Waliguswa na kisa cha ujasiri cha mtoto huyu aliyewaokoa wenzake na hapo wakaamua kuchangisha hela kiasi ili kumsaidia mamake Richard kuanza upya kutokana na hasara aliyoipata kuchomeka kwa vitu vya ndani.

Mtoto huyo wa miaka 6 alieleza kwamba japo alipoteza vitu vyake vya thamani katika moto ule kama vitabu vyake, lakini hakuona vibaya kwa sababu alifanikiwa kuwatorosha wapwa zake kutoka athari hiyo kubwa ambayo pasi na busara zake wangeangamia kwenye moto huo.

Hadithi hii ni baadhi ya hadithi nzuri tu zinazoonesha busara ya watoto wadogo katika kufanya mambo makubwa ya kuacha alama za kudumu nyoyoni mwa wengi.

Ama kweli, busara haiendi na umri!