Kumekucha! Irene Uwoya kaokoka, aalikwa kama mgeni rasmi kwenye ibada ya kanisa

Kanisa hilo litakuwa linasherehekea miaka 8 tangu kuanza huduma eneo hilo.

Muhtasari

• Mchungaji huyo alisema Uwoya ndiye atakuwa mgeni rasmi na kuzua mjadala mkali mitandaoni kuhusu wokovu wa mwanamitindo huyo.

Muigizaji na mfanyibiashara Irene Uwoya
Muigizaji na mfanyibiashara Irene Uwoya
Image: Irene Uwoya (Instagram)

Mjadala mkali umezuka miongoni mwa wanajamii ya mitandaoni baada ya mhubiri mmoja nchini Tanzania kutangaza kwamba wikendi hii atakuwa anasherehekea miaka 8 tangu kuanzishwa kwa kanisa lake na mgeni rasmi katika ibada hiyo maalum atakuwa mwanasosholaiti ambaye pia ni muigizaji Irene Uwoya.

Mchungaji huyo kwa jina Bishop Geography Bendera kwenye ukurasa wake wa Instagram alitangaza kwamba wanawake ni jeshi kubwa na hivyo jumapili hii kanisa lake la ufunuo lililoko jijini Morogoro litakuwa na ibada maalum kuwasherehekea wanawake na pia kuambatana na sherehe za kuadhimisha miaka 8 tangu aanze kutoa huduma kwa kondoo wa bwana.

“Wamama ni jeshi kubwaaaa, Jumapili hii mama wa Ufunuo Morogoro, wana jambo Lao, wakiwa na mwanamama mchapa kazi,mjasiriamali,super women @ireneuwoya8 kama mgeni rasmi,” aliandika askofu Bendera.

Askofu huyo alizidi kuelezea maana yake ya ‘super woman’ ambapo alisema huyo ni mwanamke mwenye anajitegemea na mwenye uchumi imara. Alimalizxa kwa kuwakaribisha wote kushiriki katika ibada hiyo.

“Mwanamke imara ni yule mwenye nguvu imara, woooote mnakalibishwa, Tutakula chakula pamoja "MUNGU HAJAWAHI KUSHINDWA,” aliandika Askofu.

Hatua hii ya kumpa mwaliko kama mgeni rasmi mwanamama Uowya kumezua mjadala mkali huku baadhi wakisema muigizaji huyo ameokoka na wengine wakisema kwamba Kanisa limeanza kuendekeza mambo ya hovyo kwani Uwoya anajulikana kama mwanasosholaiti ambaye uvaaji wake katika picha anazozipakia kwenye mitandao yake si za kufurahisha machoni wa watu wenye heshima.