"Kwaheri ndugu yangu, ulinileta Wasafi na sasa umeniacha" Baba levo amuaga Rayvanny

Msanii huyo chawa wa Wasafi alifichua kwamba Rayvanny ndiye aliyemleta WCB Wasafi.

Muhtasari

• Baba Levo alimuaga Rayvanny na kumtaka katu asipoteze heshima yake kwa Diamond ambaye ndiye alimbadilishia maisha.

• Jana Rayvanny alitangaza kuondoka rasmi Wasafi baada ya kudumu pale kwa miaka sita.

Wasanii Baba Levo na Rayvanny
Wasanii Baba Levo na Rayvanny
Image: Instagram

Chawa wa kampuni nzima ya Wasafi, msanii Baba Levo kama kawaida ya ndarire zake naye hajaachwa nyuma kuzungumzia suala la msanii Rayvanny kuondoka lebo ya WCB Wasafi na kuanzisha yake binafsi kwa jina Next Level Music.

Baba Levo amemuonya Rayvanny dhidi ya kuondoka na kisha kuanza kumsema vibaya babake wa kimuziki Diamond Platnumz kama ambavyo walifanya watangulizi wake Harmonize na Rich Mavoko ambao waliondoka na kukoleza ushindani kutoka nje ya pango la Diamond.

Levo alisema endapo Rayvanny atakiuka maneno hayo basi awe tayari kwa vita vya moto maana Baba Levo yeye siku zote ni mpambanaji aliyejiandaa kivita, iwe ya maneno au ya kurushiana mikwara na masumbwi.

Msanii huyo alifichua kwamba Rayvanny ndiye aliyemleta katika familia ya WCB Wasafi na sasa ameondoka na kumuacha mule, na kumtakia kila la kheri katika safari yake mpya kimuziki.

“Kwaheri ndugu yangu @rayvanny ulinileta wasafi umeniacha. Mungu akusimamie kwenye kila jambo. Hakikisha hausahau heshima uliyojengewa na @diamondplatnumz. Yeye ndio chanzo cha mabadiliko yetu kwenye maisha yetu ya muziki,” kwa mara ya kwanza Baba Levo alionekana kutema ushauri uliotukuka.

Jana Rayvanny alitangaza kuondoka rasmi kwenye lebo ya Wasafi na kumsifia pakubwa msanii Diamond Platnumz kwa kumpa nafasi ya kuonesha kipaji chake kwa dunia.

Shukrani za dhati kwa ndugu yangu Diamond Platnumz kwa kunipa nafasi dunia ione kipaji change nilichobarikiwa na mwenyezi Mungu ili kufika hapa nilipofika, kusaidia familia yangu na kufanikisha mengi katika maisha yangu,” alisema Rayvanny kwenye video ambayo aliipakia Instagram yake.

Watu wengi wamezungumzia mtindo huo wa kuondoka kwa Rayvanny na kuusifia kuwa ndio njia nzuri kabisa tena ya akili komavu kuondoka na kuacha heshima, wakijaribu kulinganisha na kuondoka kwa Harmonize miaka 3 iliyopita ambapo kulikuwa ni kuondoka kwa kivita, vurugu na jazba kubwa baina ya Harmonize na Diamond ambaye alimlea na kumkuza kimuziki.

Walimsifia Rayvanny kwa kupokezwa baraka za babake kimuziki ambaye ni Diamond Platnumz na kumtakia kila la kheri katika maisha yake kama mkurugenzi wa lebo pia.