Rayvanny adaiwa kulipa milioni 40 kupata uhuru wa kuondoka Wasafi

Mwijaku amedai Rayvanny hangeweza kufanya shoo yoyote hapo awali kabla ya kutimiza madai ya WCB

Muhtasari

•Jumanne Rayvanny alitangaza hatua yake ya kugura lebo hiyo inayomilikiwa na Diamond Platnumz katika video ya kihisia.

•Mtangazaji Mwijaku anadai kuwa Rayvanny alilazimika kulipa Tsh800M (40.5) kabla ya kuondoka WCB.

Image: INSTAGRAM// RAYVANNY

Mtangazaji na muigizaji maarufu wa Tanzania Mwijaku anadai kuwa Rayvanny alilazimika kulipa Tsh800M (40.5) kabla ya kuondoka WCB.

Jumanne Rayvanny alitangaza hatua yake ya kugura lebo hiyo inayomilikiwa na Diamond Platnumz katika video ya kihisia.

Mwijaku amedai kwamba staa huyo wa Bongo alifanya maamuzi ya kuondoka kitambo lakini akashindwa kwa kuwa aliagizwa kuacha akaunti zake za YouTube.

"Mwanzo alikuwa anapata wakati mgumu kwa sababu alitakiwa kuondoka kipindi cha nyuma lakini alitakiwa kuacha akaunti zake za YouTube alipokuwepo. Lakini akauliza pesa anazohitaji kutoa ili aondoke na akaunti zake. Akaambiwa shilingi milioni 800. Akawa anajitetea sasa," Mwijaku alisema katika kipindi cha redio.

Muigizaji huyo alidai kuwa uamuzi wa Rayvanny kuondoka uliwakera baadhi ya wasimamizi wa lebo ya Wasafi.

Alisema mtunzi huyo mahiri wa muziki hangeweza kufanya shoo yoyote hapo awali kabla ya kutimiza madai aliyopatiwa.

"Amelipa miliono 800. Huwezi kuondoka hivihivi, lazima ulipe gharama. Kwa sasa mapato yote yanayopatikana kwenye YouTube na mitandao mingine ya kisasa yatakuwa ya kwake sasa," Alisema.

Mtangazaji huyo pia alimshauri Rayvanny atafute ushauri wa Harmonize kuhusu jinsi ya kufanikiwa kama msanii huru.

Rayvanny amekuwa chini ya usimamizi wa WCB kwa kipindi cha miaka sita kufikia kuondoka kwake siku ya Jumanne.

Wakati akitangaza kuondoka kwake alishukuru uongozi mzima wa lebo hiyo  ukiongozwa na Diamondambaye pia amekuwa mwandani wake kwa kipindi kirefu.

“Miaka 6 sasa tangu tumeanza kufanya kazi pamoja na hii timu yangu, familia yangu, WCB Wasafi. Upendo, umoja vimekuwa nguzo kubwa saba kama timu. Mengi nimejifunza lakini pia mengi tumefanikisha tukiwa pamoja.. Shukrani za dhati kwa familia yangu Wasafi lakini pia kwa ndugu yangu Diamond Platnumz kwa kunipa nafasi dunia ione kipaji change nilichobarikiwa na mwenyezi Mungu ili kufika hapa nilipofika, kusaidia familia yangu na kufanikisha mengi katika maisha yangu,” Alisema katika video aliyopakia Instagram.

Rayvanny sasa atakuwa anaangazia kukuza lebo yake ya Next Level Music baada ya kupata uhuru wa kujisimamia.