"Tunapaswa kujaza dunia!" Diamond ajibu madai ya kuwa na watoto kote Afrika

"Tunapaswa kujaza dunia. Tulitumwa kufanya hivo!" Diamond alisema

Muhtasari

•Diamond aliweka wazi kuwa amewahi kupata watoto na wanawake pekee ambao alichumbiana nao kwa muda.

•Diamond alisisitiza kwamba ni wajibu wa mwanadamu kuijaza dunia kama alivyoagizwa na Mungu.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz amepuuzilia mbali madai kuwa ana watoto kote Afrika.

Akiwa kwenye mahojiano na DW Afrika, Diamond aliweka wazi kuwa amewahi kupata watoto na wanawake pekee ambao alichumbiana nao kwa muda.

"Sijawahi kupata mtoto na mtu ambaye sikutaka kupata naye ama kimakosa. Ata kama ilifanyika lazima iwe mtu ambaye tulikaa naye kwa muda, sio kimakosa," Diamond alisema.

Bosi huyo wa WCB aliweka wazi kuwa hakuna watoto wake wasiojulikana hadharani ambao alipata na wanawake wengine huko nje.

Pia alibainisha kuwa kwa kawaida huwa anaonyesha watoto wake wote kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

"Ukienda kwenye ukurasa wangu utaona huwa napakia watoto wangu pale," Alisema bila kusita.

Diamond alisisitiza kwamba ni wajibu wa mwanadamu kuijaza dunia kama alivyoagizwa na Mungu. Hata hivyo alidinda kuthibitisha idadi halisi ya watoto wake.

"Tunapaswa kujaza dunia. Tulitumwa kufanya hivo. Ni kwamba tunapaswa kuifanya vyema na kwa njjia ipasavyo. Lakini tulitumwa kuhakikisha tumejaza dunia," Alisema.

Licha ya mashaka mengi kuhusu idadi ya watoto wake, Diamond ana watoto wanne pekee wanaojulikana hadharani.

Latifah Dangote na Prince Nillan ni watoto wake wa kwanza ambao alipata na mwanasoshalaiti maarufu Zari Hassan.

Mwaka wa 2017, staa huyo alipata mtoto wa kiume na mwanamuziki Hamisa Mobetto katika kipindi kifupi cha mahusiano yao.

Baadae Diamond alijitosa kwenye mahusiano na msanii wa Kenya Tanasha na wakabarikiwa na mtoto wa kiume, Naseeb Junior, mwakani 2019.

Mara nyingi bosi huyo wa Wasafi ameshtumiwa kwa kuwapendelea zaidi watoto wake wawili wa kwanza ambao alipata na Zari.

Kwenye kurasa zake, Diamond amekuwa akiwapakia Tiffah Dangote na Prince Nillan zaidi ya wanawe wengine wawili.