(Video) Mke akoroga uji bila moto ufukweni akumuita mumewe aliyezama, kuheshimu mila

Tamaduni hiyo inasemekana ni iwapo mtu amezama na ametafutwa bila mafanikio.

Muhtasari

• Mwanaume huyo alikuwa ameenda kutafuta kuni kabla ya mkasa huo kumkuta katika ziwa Victoria.

• Mkewe alilazimika kuheshimu mila kwa kuinjika sufuria ya uji kando ya ziwa bila moto na akaanza kukoroga huku akiliita jina la mumewe.

Hivi, unaweza ukaamini kwamab watu wengi tu katika bara la Afrika bado wanaendelea kuzifuata baadhi ya mila, miiko na tamaduni za kabila zao licha ya usasa uliokuja na utandawazi na kusomba mila nyingi tu?

Nchini Tanzania, katika eneo la Kaskazini magharibi mkoa wa Mwanza, ipo familia moja iliyolazimika kuzifuata mila baada ya mpendwa wao kuzama katika ziwa Victoria mtumbwi wake aliokuwa akisafiria ulipozidiwa nguvu na mawimbi ya ziwani.

Taarifa zinasema kwamba mwanaume huyo kwa jina Salehe Haruna mwenye umri wa miaka 42 alipata ajali ya ziwani Victoria katika eneo la Sweya kweney mkoa wa Mwanza wiki iliyopita na mpaka tunaenda hewani mwili wake ulikuwa bado haujapatikana huku familia ikihofia alifariki na sasa hofu zaidi ni kuupata mwili kwa ajili ya maziko.

Kutokana na juhudi za zaidi ya wiki moja kuutafuta mwili wa Haruna bila malipo, familia ililazimika kutumia mila ambapo mkewe Haruna, Helena Misoji alitakiwa akite kambi pembezoni mwa ziwa Victoria na kuinjika sufuria kweney mafiga na kisha kuanza kukoroga uji bila moto huku akiliita jina lake.

"Hizi mila mtu akitumbukia lazima mmkorogee uji mkiita jina lake, ndugu zake kama wako unamwita, njoo unywe uji na baba yako njoo unywe uji na familia yako. Ndio mila tunafanya kusudi apatikane," mmoja wa wanajamii hiyo alisema.

Wakaazi wa eneo hilo walidai kwamba mila hiyo ilitakikana na kwamba mkewe anapofanya vile na kuliita jina lake basi mwili huo utaelea ghafla majini na kuopolewa kwa ajili ya ratiba za maziko.

Katika taarifa hizo zilizopakiwa na kurasa tofauti kutoka nchini humo, mwanaume huyo alizama ila wenzake wawili waliokuwa naye waliokolewa, Watatu hao walipatana na ajali hiyo wakati walikuwa wanatoka kutafuta kuni katika msitu wa taasisi ya uvuvi Nyegezi mkoani Mwanza.

Ajali hiyo ilitokea mnamo tarehe 13 mwezi Julai lakini baada ya siku mbili pasi na mwili wake kupatikana, mkewe aliamrishwa kutii mila hilo kama njia moja ya kusaidia mwili wa mumewe kupatikana kwa haraka.