Mbona ndoa nyingi za watu wasomi hutatizika? Mwandishi Silas Nyanchwani aeleza

Silas Gisiora Nyanchwani ni mwanahabari na mwandishi maarufu nchini Kenya

Muhtasari

• Kulingana na Nyanchwani, wanawake wengi hupenda sana kutoka kimapenzi na watu waliowazidi kwa kila kitu.

• Mwanaume ukioa mwanamke ambaye mko kiwango sawa kielimu na kipato, huenda atakuacha na kuendea mtu wa kiwango cha juu kumliko.

Mwandishi Silas Gisiora Nyanchwani
Mwandishi Silas Gisiora Nyanchwani
Image: Facebook

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na dhana mbalimbali mitandaoni kuhusu ni kwa nini ndoa nyingi za watu wasomi na wenye utajiri mkubwa huvunjika ovyo ovyo kuliko zile za watu wenye elimu ya kadri na kipato cha wastani.

Mwandishi Silas Nyanchwani anasema kwamba watu wengi haswa wanaume wasomi wenye mali elimu na mali yao huhangaika sana katika kupata ndoa na wengine kukataliwa na mbaya zaidi wengine wengi bado wanazidi kujiuguza kutokana na makovu ya kutalikiwa.

Nyanchwani anasema kwamba wengi wa wanaume hao kama wapo kwenye ndoa basi wanapitia taabu sana kwa sababu wengi wao ni watu ambao walikuwa werevu kupindukia enzi za masomo yao na sasa wako na ile dhana kwamba kila wafanyalo ni sahihi na wanahisi kudhalilishwa wakikosolewa au kupingwa katika maamuzi yao.

“Wengi wa wanaume hawa wenye maisha ya juu pengine walikuwa bora katika darasa lao. Wamezoea kuwa na kila kitu kwa njia yao. Na bado, hapa kuna kitu ambacho ni rahisi kwa udanganyifu lakini kinawaua,” alisema Nyanchwani.

Mwandishi huyo maarufu wa kitabu cha ‘Sexorcised’ anasema kwamba tatizo hili hutokana na wanaume kutaka kuoa mwanamke ambaye wako katika kiwango kimoja cha kimaisha au hata kimasomo, bila kujua kwamba mwanamke huyu kama mko kiwango kimoja basi muda wote atakuwa anahitaji maisha mazuri na mtu mwenye kiwango cha juu kumliko yeye pamoja na wewe kwa sababu mko kiwango sawa.

“Ikiwa uko kwenye ligi sawa au kiwango sawa, mwanamke atataka bora. Lakini kumbuka ikiwa wewe ni mhitimu, uko katika asilimia 0.5 ya Wakenya. Wanawake wengi wameumbwa ili kutaka wanaume bora, wenye nguvu zaidi. Ikiwa wewe ni mwanamume mwenye umri wa miaka 30 na mke kwa miaka minne na mtoto wa miaka miwili au mitatu, kuna uwezekano wa kumpoteza kwa yule mvulana bishoo wa Kijaluo au Waluhya aliye ofisini ambaye ana umri wa miaka 30 au 40. Kinachotokea ni kwamba wanawake wengi hujaribu kucheza nafasi zao na wanaume bora,” Nyanchwani alifafanua.

Kwa sasa, Nyanchwani ameachia mswada mwingine kwa jina ‘Man About Town’, kitabu ambacho kwa upana pia kinazungumzia maisha ya Wakenya wengi haswa katika mazingira ya mijini.