Mwanasiasa aandaa tafrija ya Ksh 1M kusherehekea mwaka mmoja kuzaliwa kwa bintiye

Daisy Nyongesa mwenye miaka 33 ana watoto watatu na huyo ndiye bintiye wa kipekee.

Muhtasari

• Mwanasiasa huyo alimsherehekea bintiye na kumtaja kama mrithi wake.

• Aliandaa sherehe kubwa iliyogharimu milioni moja pesa za Kenya kama njia ya kumuenzi.

Mwanasiasa Daisy Nyongesa asherehekea siku ya kuzaliwa ya bintiye kwa sherehe za 1M
Mwanasiasa Daisy Nyongesa asherehekea siku ya kuzaliwa ya bintiye kwa sherehe za 1M
Image: Instagram//honDaisyNyongesa

Aliyekuwa seneta mteule Daisy Nyongesa amekuwa mtu maarufu wa hivi karibuni kuingia kwenye orordha ya watu mashuhuri ambao waliwahi kuandaa tafrija ya kifahari kusherehekea siku za kuzaliwa za wanao.

Mwishoni mwa wiki jana, Nyongesa alishangaza wengi baada ya kudai kwamba bintiwe wa kipekee ambaye alikuwa anafikisha mwaka mmoja, shehere yake iligharimu kiasi cha milioni moja pesa za benki kuu ya Kenya.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Nyongesa alimsherehekea bintiye wa kipekee ambaye alimtaja kama mrithi wake na kusema anahisi kuwa mbarikiwa kuwa na watoto watatu akiwa na umri wa miaka 33 tu.

“Heri njema ya siku yako ya kuzaliwa binti wangu wa kipekee na mrithi wangu Eunice Zawadi Mwenje. Ujio wako ulikamilisha mduara wa familia hii, wewe ni mtoto niliyeomba. Wewe ni kiumbe kizuri kilichotengenezwa kwa mikono na Mungu, umewekwa mikononi mwangu nikukuze, kukupenda, kukutunza na kukuenzi kama rafiki yangu wa maisha,” Nyongesa aliandika.

Mwanasiasa huyo alisema kwamba tabasamu la bintiye hiyo ni la kufana sana na kudokeza kwamba hata hakuona vibaya kutumia kima cha shilingi milioni moja kumsherehekea anapotimiza mwaka mmoja tangu kuzaliwa.

“Tabasamu lako linapendeza, kicheko chako kinaambukiza, hakika wewe ni hazina yangu kuu na ningeitoa dunia nikiweza kwa sababu ulitumwa kuniokoa, sasa nina nguvu na hekima zaidi. Ndio maana nilihisi tafrija ya shilingi Milioni Moja itakuwa zawadi bora kwako unapotimiza mwaka mmoja,” Ngongesa alitokwa na maneno ya furaha.

Mwanasiasa huyo si mtu mashuhuri wa kwanza kurusha tafrija la kiwango cha nyota tano kusherehekea wanao kwani miezi michache iliyopita wakati Asia brown, mwanawe aliyekuwa mwanasosholaiti Vera Sidika na mwanamuziki Brown Mauzo alikuwa anatimiza nusu mwaka, wachumba hao walimsherehekea na mpaka kumfungulia biashara ya mafuta ya kupaka watoto kuwa mkurugenzi mkuu akiwa na miezi sita tu duniani.

Wengine ambao pia waliwahi kuwasherehekea wapendwa wao kwa tafrija ghali ni pamoja na naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe qambaye alisherehekea miaka 28 ya bintiye kwa hafla ya kufana, Akothee akisherehekea siku ya kuzaliwa ya bintiye Vasha, Mchungaji Carmel aliwahi kumnunulia vipande viwili vya mashamba mpenzi wake mchungaji Lucy Natasha miongoni mwa watu wengine maarufu.