Tiktoker aliyedaiwa kuathirika vibaya baada ya kula buibui hatimaye aweka wazi yaliyojiri

Aq9ine amekiri kuwa hakuugua baada ya kula buibui.

Muhtasari

•Aq9ine amesema hakula buibui ila mnyama huyo mdogo hatari ndiye aliyemuua kwenye mkono wake wa kushoto.

•Aq9ine alisema wasiwasi uliomwingia baada ya kung'atwa na buibui ndio uliomfanya kudai kuwa aliathirika baada ya kumla.

Image: INSTAGRAM// AQ9INE

Mtumbuizaji maarufu wa Tiktok Aq9ine hatimaye amejitokeza kufafanua kuhusu kisa ambapo ilidaiwa aliugua sana baada ya kula buibui.

Mapema mwezi huu Aq9ine alipakia video ya kutisha iliyoonyesha uso na mikono yake ikiwa imevimba vibaya.

Tiktoker huyo ambaye huwatumbuiza wanamitandao kwa kujaribu vyakula mbalimbali vya ajabu alisema aliugua baada ya kula buibui.

"Ikiwa hii ndio video yangu ya mwisho, imekuwa jambo la kufurahisha kuwaburudisha na kuhatarisha maisha yangu pia. Ninapenda hatari sababu tunaishi hatari. Sisi sote tutakufa. Nawapenda sana ndugu zangu," Aq9ine aliandika chini ya video hiyo ambayo alipakia kwenye Instagram.

Katika video hiyo, Aq9ine  alielezea  dalili alizokuwa nazo huku akionyesha jinsi mwili wake ulivyoathirika.

"Wadau,, nifanyieni maombi ya mwisho kabla niende. Mniombee tu bana mi naenda. Nasikia ni kama sina uso, nafura tu. Mazee nimekula buibui bana. Hii inafanyikia uso wangu. Nifanyieni maombi ya mwisho," Alisema.

Aq9ine alionekana mwenye maumivu makali na wasiwasi mwingi. Pia alishinda akijikuna kwenye uso na mikono.

Video hiyo ilialika hisia mseto kutoka kwa wanamitandao huku wengi wao wakimtakia afueni na  wengine wakimkosoa.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, mchekeshaji huyo kutoka Meru hata hivyo amefichua kuwa hakuugua baada ya kula buibui.

Ameeleza kuwa hakula buibui ila mnyama huyo mdogo hatari ndiye aliyemuua kwenye mkono wake wa kushoto.

"Mimi sikula buibui, ilinikula. Niliumwa na buibui mkononi wakati tulikuwa tunaenda kazi na foreman wangu. Huwa nafanya mjengo. Niliumwa nikiwa Chogoria," Aq9ine alisema katika mahojiano na Nicholus Kioko.

Mtumbuizaji huyo alidai kuwa alijawa na wasiwasi na uchungu mwingi mwilini baada ya kung'atwa na buibui.

Alisema kuwa alivimba sehemu zote za mwili wake ikiwa ni pamoja na usoni, mikononi, miguuni, mgongoni na tumboni.

"Nilikuwa nimefura. Ilikuwa kitu serious. Nilikuwa pabaya. Nilikuwa nimefura kila mahali. Lakini nilihudumiwa. Sikukanyanga  hospitali. Nilihudumiwa nyumbani," Alisema.

Aq9ine alisema wasiwasi mwingi uliomwingia baada ya kung'atwa na mnyama huyo ndio uliomfanya kuibua madai kuwa aliathirika baada ya kumla.

"Mimi nikifanya video nilikuwa ni na wasiwasi. Kwa hivyo ata sikujua chenye nilisema. Nilirudi kushangaa baadae baada ya video kuenezwa kila mahali," Alisema.

Pia alipuuzilia mbali madai kuwa alikarabati video hiyo ili kuonyesha kama mwamba  alikuwa anaugua.

Aidha, mtumbuizaji huyo alisisitiza kuwa anatazamia kumpika na kumla nyoka katika siku zijazo.