Diana Marua afunguka kwa nini anataka Bahati afanyiwe upasuaji wa kufunga uzazi

Diana aliweka wazi kuwa kufikia hatua hii hawezi kustahimili ujauzito mwingine.

Muhtasari

•Diana ameonyesha wazi kuwa  ameridhika na watoto wanne ambao anawalea tayari  pamoja na yule aliyebeba tumboni.

•Diana ametoa ombi kwa mumewe Bahati kufanyiwa utaratibu wa kufunga uzazi unaojulikana kama Vasectomy.

Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwanavlogu na mwimbaji maarufu Diana Marua amedokeza kuwa ujauzito anaobeba kwa sasa utakuwa wake wa mwisho.

Diana ameonyesha wazi kuwa  ameridhika na watoto wanne ambao anawalea tayari  pamoja na yule aliyebeba tumboni.

"Mimi nadhani nimefunga ukurasa wa kuzaa. Ni mwisho. Niko na watoto watano. Katika hatua hii tumefunga!," Diana alisema katika mahojiano na Eve Mungai.

Rapa huyo anayefahamika kwa jina la jukwaani Diana B aliweka wazi kuwa kufikia hatua hii hawezi kustahimili ujauzito mwingine.

Kutokana na hayo ametoa ombi kwa mumewe Bahati kufanyiwa utaratibu wa kufunga uzazi unaojulikana kama Vasectomy.

"Bahati anafaa aende kufanyiwa Vasektomi kwa sababu katika hatua hii, huko ndiko kujitolea pekee anakoweza kwa ajili yangu. Yeye aende afunge vitu zake. Mimi nimejitolea sana kwa ajili yake. Nimembebea watoto, huyu ni watatu, miezi tisa kwa kila mtoto. Sasa yeye aende afunge tumalize," Alisema.

Ujauzito anaobeba msanii huyo kwa sasa ni wake wa tatu. Tayari amejifungua watoto wengine wawili, Heaven Bahati na Majesty Bahati.

Diana na Bahati pia wamejipa jukumu la kuwalea watoto wengine wawili, Morgan Bahati ambaye alichukuliwa kutoka nyumba  ya watoto na Mueni Bahati ambaye ni mtoto wa Bahati na aliyekuwa mpenzi wake, Yvette Obura.

Katika mahojiano hayo ya Youtube, mama huyo wa watoto wawili pia alifichua kuwa mumewe huwa na hamu kubwa ya tendo la ndoa.

Hapo awali Bahati hata hivyo alikuwa amelalamika kuwa mkewe amekuwa akimnyima haki zake za ndoa.

Diana alijitetea kwa kusema,"Baha sasa ni mhesh. Anashinda kwa ground. Mimi nimechoka, nimebeba mtoto, anataka aniamshe saa nane akuje atoe stress zake  na mimi. Huwa namwambia asubiri asubuhi. Asubuhi akifika ako na shughuli zake, nami niko na zangu. Kuna hiyo lakini tutajaribu," Alisema.

Mtumbuizaji huyo wa YouTube pia alifichua kuwa ujauzito wake wa tatu ulimpata kwa mshangao kwani hakuutarajia.

Alikiri kuwa yeye na mumewe Bahati hawakuupangia ujauzito huo na ndiposa alichukua muda  kabla ya kutangaza.

"Sikukaa chini nikasema nataka Heaven ama Majesty. Ujauzito wa Heaven na Majesty ulikuwa umepangwa. Hii ingine ilibackfire. Ilikuwa mshangao," Diana alisema.