(Video) Mwanaume, 27, ateta kunyimwa kazi kutokana na muonekano wake wa kitoto

Mwanaume huyo alisema anabaguliwa na waajiri watarajiwa kutokana na maumbile yake kama mtoto wa chini ya miaka 10 ilhali ana umri wa miaka 27.

Muhtasari

• Wanamtandao waliwakosoa wanaotaka kuwa waajiri kwa kutompa Mao nafasi ya kujithibitisha kwa sababu tu ya jinsi anavyoonekana.

Mwanaume mmoja kutoka Uchina kwa jina Mao Sheng amezua gumzo mitandaoni baada ya kudai kwamba ameshindwa kupata kazi kutokana na waajiri watarajiwa kumuona kama mtoto na hivyo kumyima kazi.

Mao Sheng mweney umri wa miaka 27, kutoka mkoa wa Guangdong, Uchina, ana kimo kidogo na mwonekano wa ujana. Alisema jinsi anavyoonekana ni tatizo kubwa katika maisha yake kwani wengi wa waajiri watarajiwa wanachukulia kama mtoto na hilo limesababisha yeye kukosa nafasi nyingi za kazi. Kwa muonekano wa nje, anaonekana mtoto wa umri wa chini ya miaka 5.

Kulingana na taarifa zilizochapishwa na majarida ya nchini humo, Mao alisema kuwa waajiri watarajiwa hawamwamini anapowaambia umri wake. Wengine wanafikiri kuwa mwonekano wake utasababisha matatizo na mamlaka ambazo zinaweza kuanza kuchungulia iwapo zinafikiri sheria za kuwaajiri watoto zinavunjwa.

Mwanaume huyo mwenye alichapisha video yake akionyesha kufadhaika kwake kwamba hawezi kumsaidia babake kifedha kwa sababu hawezi kupata kazi. Mao alisema kwamba alikuwa ametoka kutafuta kazi na rafiki yake ambaye alipata kazi hiyo haraka lakini hakupokea ofa yoyote.

Katika video nyingine, alionyesha kitambulisho chake ambacho kilisema kwamba alizaliwa mnamo mwaka 1995.

Alieleza kwamba baada ya mama yake kuolewa tena na baba yake kupata kiharusi, Mao ndiye anabaki kuwa tegemezi la pekee wa baba yake, na anaponyimwa kazi kutokana na umbile lake kunazidisha mfadhaiko kwa baba yake ambaye anaugua.

Mao alipoambiwa kuhusu video hiyo kusambaa mitandaoni, alikuwa na wasiwasi kwamba familia yake ingemkasirisha. Alihofia kuwa huenda klipu hiyo ikafanya ionekane kama hakuwa akichukua kazi hiyo kwa uzito.

Wanamtandao waliwakosoa wanaotaka kuwa waajiri kwa kutompa Mao nafasi ya kujithibitisha kwa sababu tu ya jinsi anavyoonekana.

Hata hivyo, tangu video hiyo kusambaa, Mao pia alipokea idadi ya waajiri wanaoweza kumfikia.

Inasemekana alikubali moja ya ofa.