"Wee Oolisikia wapi?" Mbunge wa Tanzania kuja Kenya kumpigia Raila kampeni

Mbunge Selemani Said Bungara alitrend sana Kenya kwa maneno yake ya "Wee oolisikia wapi?"

Muhtasari

• Chama chake cha ACT Wazalwendo kiliweka taarifa hiyo wazi kwa umma na kusema kwamba mbunge huyo anakuwa wa kwanza kabisa kutoka nchi hiyo kupewa heshima kuhudhuria mkutano wa kisiasa nchini Kenya.

Mgombea urais wa Azimio Raila Odinga na mbunge wa zamani wa Kilwa Kusini, Tanzania, Ndugu Selemani Said Bungara (Bwege)
Mgombea urais wa Azimio Raila Odinga na mbunge wa zamani wa Kilwa Kusini, Tanzania, Ndugu Selemani Said Bungara (Bwege)
Image: Facebook (Raila Odinga), YouTube (NTV Screenshot)

Taarifa kutoka nchini Tanzania zinaarifu kwamba Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Kilwa Kusini na aliyekuwa Mgombea wa Jimbo hilo kwa tiketi ya ACT Wazalendo kwenye Uchaguzi Mkuu 2020 Ndugu Selemani Said Bungara (Bwege) yupo safarini kuja nchini Kenya kushiriki mkutano mkuu wa kampeni za muungano wa Azimio la Umoja One Kenya zitakazofanyika Jumapili katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani.

Katika taarifa zilizochapishwa kweney ukurasa wa Facebook wa chama cha ACT Wazalendo na ambazo zimesambazwa pakubwa kwenye mitandao ya kijamii ndani na nje ya nchi hiyo Jirani, Janeth Rithe ambaye ni Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama hicho alisemekana kutoa taarifa hiyo na kuifuatisha na picha ya mbunge huyo akiwa anashuka ndege katika ang atua.

TAARIFA KWA UMMA. Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Kilwa Kusini na aliyekuwa Mgombea wa Jimbo hilo kwa tiketi ya ACT...

Posted by ACT Wazalendo on Wednesday, August 3, 2022

Selemani Said Bungara, ama Bwege kwa jina lingine alijizolea umaarufu mkubwa nchini Kenya miaka miwili iliyopita kutokana na mitikasi yake ndani na nje ya bunge la Jamhuri ya Tanzania kwa kauli alizokuwa akizitoa kwamba ‘Wewe ulisikia wapi?” kauli ambayo ilidakiwa na wakenya wengi mpaka wengine kuchapisha tisheti zenye maneno hayo.

“Ndugu Bwege ndio Mwanasiasa wa kwanza kutoka Tanzania kupewa heshima hiyo na Timu ya Kampeni ya Azimio la Umoja. Kumbukumbu za mtandaoni zinaonesha kuwa hotuba za Ndugu Bwege ndani na nje ya Bunge zinafuatiliwa na kupendwa sana Nchini Kenya,” Janeth Rithe alinukuliwa kweney taarifa hiyo.

Nchini Kenya, uchaguzi unatarajiwa kufanyika Jumanne wiki kesho na kampeni zote zinafaa kutamatika siku mbili kabla, kulingana na katiba ya mwaka 2010, ambayo ni siku ya Jumapili na mirengo mbalimbali imeweka mipango Madhubuti kuhitimisha siku hiyo ya mwisho ya kujinadi katika makongamano ya kitaifa sehemu tofauti jijini Nairobi.