Jamaa aelezea jinsi aliibuka kutoka familia ya kimaskini na kuwa mhandisi UK

Alisema alitia bidii kuwa namba moja darasani, hangeweza kuwa namba 2 sababu vitabu vyake vilikuwa tegemeo la kufunza wadogo zake ambao hawangeenda shule juu ya karo.

Muhtasari

• "Mimi ni mtoto wa kwanza wa familia ya Kiafrika. Nimekuwa na shinikizo kutoka siku ya kwanza,” mwanaume huyo alieleza.

Toyyib Adewale Adelodum , mhandisi aliyesimulia jinsi alipata kazi Uingereza.
Toyyib Adewale Adelodum , mhandisi aliyesimulia jinsi alipata kazi Uingereza.
Image: Twitter//Toyyib Adewale Adelodum

Mwanaume mmoja kweney mtandao wa Twitter amegusa mioyo ya wengi baada ya kuelezea jinsi alivyopata kazi ughaibuni baada ya kupitia mateso mengi katika maisha yake ya ukuaji.

Toyyib Adewale Adelodum aliandika kwenye Twitter yake na kuelezea kwamba hatimaye baada ya uteseka kwa kipindi kirefu tangu kuzaliwa kwake, alifanikiwa kupata kazi katika shirika moja Uingereza baada ya kuulizwa swali la kizushi kwamba uzuri na ubora wake katika kufanya kazi chini ya shinikizo ni wa kiwango kipi.

Alisema aliwajibu kwamba yeye muda wote amekuwa akifanya kila kitu chini ya shinikizo na kusema hilo ndilo lilimsaidia kupata kazi.

“Niliingia kwenye usaili kufanya kazi katika kampuni ya moja ya uhandisi Uingereza. Waliniuliza swali, "vipi unafanya kazi kwa shinikizo?" niliwaibu kwamba Mimi ni mtoto wa kwanza wa familia ya Kiafrika. Nimekuwa na shinikizo kutoka siku ya kwanza,” mwanaume huyo alijibu.

Adelodum alizidi kuelezea kwamba maisha yake tangu kuzaliwa yamekuwa yakiratibiwa na matukio ya shinikizo hadi kuzxoea, kwani siku zote dhiki ikizidi pima huonekana nyanda tu!

Alifichua kwamba hata shule ya msingi aliyoisomea ilikuwa ni shule ambayo wazazi wake hawangeweza kuimudu licha ya kuwa shule ya kawaida mno.

Pia alidokeza kwamba hili lilimpa msukumo wa kuwa wa kwanza muda wote katika darasa lao kwani vitabu vyake vilikuwa vinategemewa na wadogo zake ili kujifunza kule nyumbani kwa sababu hawangeweza kuenda shule kutokana na ugumu wa kupatikana kwa karo.

Alisema baada ya kujieleza hivyo kwa hamasa kubwa, hakutoka nje ya ua la kampuni ile kabla ya kudhibitishiwa kwamba kazi ameipata. Aliwashauri watu kutoogopa kuelezea hadithi ya maisha yao wanaposailiwa kwa kazi.

“Nilisoma shule ya msingi ambayo wazazi wangu hawakuweza kumudu. Kwa hivyo ilinibidi kuwa wa kwanza darasani kila muhula ili kuendelea na masomo. Vitabu vyangu vilitumika kufundisha ndugu zangu nyumbani, walikuwa hawawezi kuenda shule, kwa hivyo sikuweza kumudu kuwa wa 2 darasani. Sikutoka kwenye kiwanja kabla hawajapiga simu kwamba nimepata kazi. Kumbuka kusimulia hadithi yako” Adelodum aliendelea kuelezea.