Mabwenyenye wa Tanzania walitoa Ksh12M kwa Diamond kutumbuiza Kasarani

Muungano wa Azimio uligharamia safari ya Diamond kutoka Afrika Kusini hadi Kasarani.

Muhtasari

•Diamond ndiye alikuwa msanii mgeni maalum kwenye mkutano wa mwisho wa Azimio la Umoja-One Kenya.

•Azimio ililipia gharama zilizotokana na ndege yake ya kibinafsi na pia chopa iliyomfikisha uwanjani.

Mgombea urais Raila Oinga na staa wa Bongo Diiamond Platnumz
Image: EZEKIEL AMING'A

Staa wa Bongo Diamond Platnumz alivuna takriban shilingi milioni 12 kutoka kwa shoo yake ya dakika chache katika uwanja wa Kasarani mnamo Jumamosi.

Diamond ndiye alikuwa msanii mgeni maalum kwenye mkutano wa mwisho wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Bosi huyo wa WCB alitua nchini kutumia ndege yake ya kibinafsi kisha kuchukuliwa na chopper ya Azimio hadi kwenye uwanja wa Kasarani.

Chanzo kilichozungumza na Radio Jambo kimearifu kuwa Azimio iligharamia safari yake kutoka Afrika Kusini alikokuwa hadi Kasarani. Muungano huo ulilipia gharama zilizotokana na ndege yake ya kibinafsi na pia chopa iliyomfikisha uwanjani.

"Azimio alilipia chopper yake tu, alilipwa milioni 12 na vigogo wa Tanzania kutumbuiza kwa dakika tatu," Mtu aliye na maelezo ya shoo hiyo alisema. 

Diamond aliwasisimua wafuasi wa Azimio waliokuwa wamejumuika Kasarani Jumamosi kwa matumbuizo yaliyodumu kwa dakika chache tu. Kati ya ngoma zake alizocheza ni pamoja na Babalao, Amaboko na Waah kabla ya Raila kuungana naye jukwaani.

Wakati wa shoo hiyo, Diamond pia alimpigia debe waziri huyo mkuu wa zamani na huku akisema  nchi hiyo inamwaminia  kuwa rais.

"Nataka nikuambie vijana wanakuamini sana, nchi inakumaini sana, na wewe ndiye Rais unayefuata," Diamond alisema.

Alilipanda jukwaa akiwa amevalia vesti nyeupe,  suruali ya jeans na kitambaa cheupe kichwani. Pia aliambatana na wacheza densi waliovalia vesti nyeupe.

Baada ya hotuba ya Raila, Diamond alirejea jukwaani na kutumbuiza kidogo kabla ya kuondoka na kurudi Afrika Kusini akiwa ameandamana na binti yake Tiffah Dangote.

Baadae msanii huyo alijumuika na familia yake kusherehekea siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Tiffah.