(+video) "Sipigi Kura, Raila Aliwapa Diamond na Mbilia Bel Pesa Yote" - Okoth Vicky, Mwanamuziki

Tafakari kwamba sina nauli na Raila Odinga alimpa Diamond Platnumz pesa zote milioni 10 akaenda - Okoth Vicky

Muhtasari

• “Mafuta sina na Raila Odinga anataka nimpigie kura, unga wangu umebaki kidogo, kila kitu kimeisha hapa, sasa mimi nitampigiaje kura na alipatia Mbilia Bel na Diamond pesa yote" - Okoth Vicky

Mwanamuziki Okoth Vicky aliyetamba na kibao Firimbi Movement akiimbia mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga amekuwa msanii wa hivi punde kuteta vikali kutokana na hatua ya muungano huo kuwaleta wasanii wa kigeni kutumbuiza katika mikutano yao ya kisiasa huku wakiwatenga wasanii wa humu nchini.

Katika video ya msanii huyo ambayo imesambazwa mitandaoni, Okoth Vicky anaonekana akilalama na kuapa kwamba safari hii hataenda kupiga kura kwani hana hata nauli ya kumfikisha nyumbani ili kumpigia Raila Kura.

“Mwaka huu siendi kupiga kura kwa sababu niliachia ngoma tisa za kampeni kwa Raila Odinga lakini siendi kumpigia kura kwa sababu mwanzo sina nauli ya kunitoa Kakamega mpaka Kisumu kupiga kura. Tafakari kwamba sina nauli na Raila Odinga alimpa Diamond Platnumz pesa zote milioni 10 akaenda, kitu hicho hicho ambacho alifanya kwa Mbilia Bel akarudi kwao, sasa mimi Raila Odinga anataka nimpigie kura, wacha Diamond na Mbilia Bel wampigie kura,” Okoth Vicky anaonekana akiteta vikali.

Msanii huyo alizidi kuelezea na hata kuonesha mashabiki wake kwa video kwamba hana kitu cha kula katika rafu yake kuanzia ufuta wa kupika hadi unga na kusema kwamba Raila Odinga hajawatendea haki kwa kuwataka waende kumpigia kura huku pesa zote akiwalipa wasanii kutoka nje.

“Mafuta sina na Raila Odinga anataka nimpigie kura, unga wangu umebaki kidogo, kila kitu kimeisha hapa, sasa mimi nitampigiaje kura na alipatia Mbilia Bel na Diamond pesa yote. Sina hata chakula cha leo, nitakupigiaje kura baba? Unasema wewe utasaidia wasanii wa humu ndani na bado unawasapoti wasanii wa nje, wewe na Atwoli, sasa unaona…” Okoth alilalama.

Msanii huyo ambaye alidokeza kwamba amemfanyia Raila ngoma nyingi za kampeni bila malipo amekuwa wa hivi punde kuweka kwenye mizani suala la Diamond kuja nchini na kutumbuiza katika mkutano wa mwisho wa kisiasa wa muungano wa Azimio la Umoja ugani Kasarani Jumamosi iliyopita, huku kukiwa kumeibuka makundi mawili, moja likitetea hatua ya Diamond kualikwa na kutumbuiza huku wengine wakionekana kutofautiana kwamba nafasi hiyo ingepewa kwa wasanii wa humu nchini.