(+VIDEO) "Msiniite Harambee Zenu, Mlitumia Pesa Zangu na Hamkunichagua" Mwanasiasa Alia

“Maisha lazima yaendelee, nina maisha ya kuishi, Harambee naomba ujiweke, usiniite tena” alisema.

Muhtasari

• "Nimetumia rasilimali zangu zote, nimekuwa nikiweka akiba, hata HELB yangu, tangu nikiwa chuoni, nikiweka akiba kwa ajili ya uchaguzi huu," alisema.

Kijana mmoja ameiuka mitandaoni akidai kwamba alikuwa akigombea wadhifa wa mjumbe wa kaunti, MCA katika kaunti ya Meru ila watu walimuangusha licha ya kutumia mtaji wake wote ikiwemo mkopo wa kufadhili masomo ya vyuo vikuu, HELB.

Katika video ambayo aliipakia mitandao ya kijamii na ambayo imezungumziwa sana kwa njia tofauti, kijana huyo kwa jina Festus Kithinji analalama kwamba alibwagwa chini kwa kishindo katika kinyang’anyiro cha udiwani, Mbeu kwa tikiti ya chama cha Wiper kilichoko chini ya mwavuli wa Azimio la Umoja One Kenya.

Alisema jinsi alivyojisikia kuchezewa shere na wapiga kura waliokuwa wakimmiminia sifa kochokocho na kuzimega pesa zake, kiasi kikubwa akisema kilikuwa mtaji wake ambao aliwekeza kwa muda mrefu kutoka kwa mkopo wa HELB ambao alikuwa akipokea kila mwaka akiwa chuo kikuu.

"Nimetumia rasilimali zangu zote, nimekuwa nikiweka akiba, hata HELB yangu, tangu nikiwa chuoni, nikiweka akiba kwa ajili ya uchaguzi huu," alisema.

Alisema alihisi kudanganywa kwani alikuwa akiongoza takriban kura zote za maoni lakini matokeo ya kura halisi yalikuja tofauti.

"Nilikuwa naongoza kulingana na kura za maoni, lakini dakika ya mwisho unaamua tu kumpa mtu kwa sababu ya pesa, hiyo sio haki kwangu," Kithinji anaonekana akilalama kwa uchungu.

“Ninavyosimama hapa akaunti yangu inasoma sifuri, niliweka juhudi zangu zote pale nikidhani mnanipa kura, hivi, nyie watu waongo, kwanini mlinidanganya kuniita mheshimiwa, kumbe mlijua hamtanipa kura zenu," alipandwa na mori.

Pia alikuwa na uchungu kwamba baadhi ya vituo vya kupigia kura hakupata kura hata moja huku wengine wakimwambia kuwa 2027 itakuwa bora zaidi.

"2027 itakuwa bora, bora kwa njia gani, watu watakuja na pesa na siwezi kuahidi nitakuwa na pesa za kutosha kwa ajili yenu. Kwa kweli ninahisi kuangushwa na kuvunjwa moyo sana, nahisi kabisa kama nitaacha siasa kabisa, ni vibaya sana"

Aliapa kwamba sasa ashagundua siasa na pesa vinatangamana na sasa Kwenda mbele anaenda kutafuta pesa kwa wingi ili uchaguzi ujao akuje kwa kishindo cha zilizala.

“Maisha lazima yaendelee, nina maisha ya kuishi, siasa si suala la kufa na kupona, ukiwa na Harambee naomba ujiweke, usiniite tena” alisema.