Mama wa watoto 6 aliyekuwa mfungwa jela apata digrii ya Uzamili ili kuwatia moyo wanawe

"Haijalishi unapoanzia, lakini unapoishia ndicho chenye umuhimu mkubwa tena wa kudumu." - Hall anawashauri watu

Muhtasari

• Hall, mama wa watoto 6 na mweney umri wa miaka 47 alijibidiisha mpaka kupata digrii 3 ndani ya miaka 5.

Margaret Hall, 47 mama wa watoto 6 aliyepata shahada tatu ndani ya miaka 5 licha ya kuwa mfungwa
Margaret Hall, 47 mama wa watoto 6 aliyepata shahada tatu ndani ya miaka 5 licha ya kuwa mfungwa
Image: Jarida la Black Women

Jarida moja la Black Women nchini Marekani limeangazia hadithi ya mwanamke mmoja mfungwa ambaye ameenda nje ya uwezo wa kawaida na kuhakikisha amesoma mpaka kupata shahada ya uzamili licha ya kuwa mfungwa gerezani.

Mwanamke huyo kwa jina Margaret Hall mhalifu mwenye umri wa miaka 47 kutoka maeneo ya Arizona ni mama wa watoto sita na alihitimu kwa shahada hiyo ambayo ni yake ya tatu chini ya miaka mitano, kwa kile alisema kwamba watoto wake ndio walimpa himizo na motisha ya kusoma hadi upeo wa juu zaidi.

Hall alihukumiwa kifungo cha miezi 6 katika gereza la shirikisho kwa makosa ya daraja la C ila sasa kutokana na kutaka kufifisha picha katika macho ya wengi ambao walikuwa wanamuona kama mhalifu, alizamia masomo na kuhitimu na shahada ya uzamili katika masomo ya sheria za Kitaaluma kutoka chuo cha kikuu cha jimbo la Arizona.

Jarida hilo linaripoti kwamba Margaret alijiandikisha awali katika chuo cha jumuiya ya eneo hilo kwa sababu alihisi kuogopa kuwa mhalifu. Walakini, baada ya kusoma kwa bidii na kupata ufadhili wa masomo, alianza kujiamini zaidi na hivi karibuni akahamishiwa ASU. Anasema kwamba alikuwa darasani kila muhula kwa miaka 5 iliyopita bila majira ya joto na hakuna mapumziko.

Motisha yake ilikuwa nini? Aliazimia sana kuwatia moyo watoto wake. Anasema, "Sikutaka watoto wangu wafikiri kwamba hiyo ingekuwa sura ya mwisho ya hadithi yangu." Pia alitoa ushauri wenye nguvu kwa wengine ambao wanaweza kuwa katika hali sawa na iliyomkuta kwa kuwausia kauli mbiu kwamba, "Haijalishi unapoanzia, lakini unapoishia ndicho chenye umuhimu mkubwa tena wa kudumu."

Kuhusu maisha yake ya baadaye, anasema kwamba anataka kuanzisha biashara ya uandishi wa ruzuku ili kusaidia mashirika yasiyo ya faida ambayo husaidia wengine kupata mafanikio.