"Nililewa sana nikazimia, kuamka nikajipata kwenye jeneza" Jamaa aeleza

Alidai kwamba alikuwa ametolewa kafara kwa miungu

Muhtasari

• Mwanaume huyo alidai kwamba alipovunja glasi ya jeneza uchafu ulianza kuingia ndipo aligundua kwamab alikuwa amefukiwa.

Víctor Hugo Mica Álvarez jamaa aliyelewa na kujipata ndani ya jeneza amezikwa
Víctor Hugo Mica Álvarez jamaa aliyelewa na kujipata ndani ya jeneza amezikwa
Image: New York Post

Mwanaume mmoja nchini Bolivia, Amerika ya Kusini alieleza kisa cha kusikitisha kuhusu kile alikitaja kuwa alitolewa kama dhabihu ya msukule baada ya kuenda katika tafrija ka kulewa chakari na baadae kuamka akiwa kwenye jeneza.

Jamaa huyo alielezea kwamab alijaribu kuwaeleza vyombo vya dola jambo hilo ila wakampuuzilia mbali kwa kusema kwamba bado huenda anasumbuliwa na ulevi kichwani unaomfanya kutunga hadithi hizo ambazo kwao zilikuwa kama hekaya za abunuwasi na kumtaka kuenda nyumbani, alikaidi na kuamua kupasua mbarika kwa vyombo vya habari nchini humo.

Kulingana na jarida la New York Post, Víctor Hugo Mica Álvarez mwenye umri wa miaka 30 alialikwa kuhudhuria tamasha la Mama Dunia huko El Alto, Bolivia, mnamo Agosti mosi ambapo tukio hilo lilimtokea, katika kile alisema ilikuwa njama ya kumtoa kafara kinyume na matakwa yake.

Álvarez alikuwa mgeni katika hafla ya kila mwaka, ambapo vikundi vya asili hukusanyika kumwabudu Mungu wa kike Pachamama kwa kumtolea sadaka.

“Álvarez anadai kuwa alikuwa akinywa pombe kupita kiasi wakati wa tamasha na baadaye akazimia. Saa kadhaa baadaye, aliamka na hamu ya kukojoa - ndipo akagundua kuwa alikuwa amelala ndani ya jeneza la glasi, lililofunikwa na uchafu,” jarida la New York Post liliripoti.

"Kitu pekee ninachokumbuka ni kwamba nilidhani niko kitandani mwangu na nikainuka kwenda kukojoa, na sikuweza kusonga. Niliposukuma jeneza sikuvunja glasi kwa shida na, kupitia glasi, uchafu ulianza kuingia," Alvarez alidai kwa uchungu.

Mwanaume huyo katika kile kinaonekana kama hadithi ya kubuni ila yeye anasema ni kitu cha kweli kilichomtokea alisema kwamba baada ya kujisatiti kwa muda kiasi, aliweza kutoka na kudai kwamab alikuwa amezikwa kaam njia moja ya kutolewa sadaka kwa miungu.

Kulingana na jarida lingine la Metro, mara baada ya Alvarez kupata fahamu zake, aligundua kuwa alikuwa amesafirishwa hadi sehemu moja kwa jina Achacachi - kama maili 50 kutoka ambapo alikuwa amekunywa mwanzoni mwa tamasha.

Picha zilizopigwa na vyombo vya habari zinamuonyesha akionekana kuwa na damu na michubuko baada ya madai ya kutoroka. Wakati huohuo, Metro imeripoti kwamba Alvarez hana shaka kwamba alitolewa kuwa dhabihu ya kwa Pachamama, akisema: "Walitaka kunitumia kama sullu."

Chapisho hilo linadai kwamba "sullu" ni bidhaa inayotolewa kwa mungu wa kike, pamoja na peremende, mimea ya dawa, mayai na madini ambayo kwa kawaida hukabidhiwa.