Polisi waliomkamata Bi Harusi kwa wizi wa pesa kushtakiwa kwa kuvuruga harusi

Polisi hao walikatisha sherehe ya arusi baada ya kumkamata bibi arusi na kuondoka naye kituoni.

Muhtasari

• Msemaji wa polisi alisema polisi hao hawakutumwa na yeyote kumkamata mwanamke huyo na kusema watachukuliwa hatua.

• Alisema tayari afisa aliyekuwa anachunguza kesi hiyo amekamatwa huku wengine walioshirikiana naye kuvuruga harusi wakiwa mbioni.

Msemaji wa polisi nchini Uganda
FRED ENANGA Msemaji wa polisi nchini Uganda
Image: Twitter

Wikendi iliyopita, video ya polisi nchini Uganda wakimtia nguvuni bibi harusi katika siku ya tukio lake kubwa ilisambazwa mitandaoni huku ikivutia maoni kinzani kutokana na jinsi polisi hao walionekana wakimburuza na kuenda naye.

Katika kujitetea, polisi hao walisema kwamba mwanamke huyo ambaye siku ya tukio alikuwa amepambwa kama bibi harusi mtarajiwa alikuwa ameiba na kutoroka na pesa kutoka sehemu moja alikokuwa akifanya kazi.

Ila tukio hilo la jinsi maafisa wa polisi walimnyanyua juu kwa juu lilizua ghadhabu miongoni mwa wananchi ambao wengi walitaka kupata majibu kutoka wakuu wa polisi nchini humo.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti moja la nchini humo leo, msemaji wa polisi aliyetambuliwa kwa jina Fred Enanga alisema kitendo hicho kilikuwa cha kuchukiza na kusema polisi husika watachukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu.

Gazeti hilo lilimnukuu Enanga akisema kwamba tayari baadhi ya polisi husika wametiwa nguvuni huku wengine ambao bado wamo mafichoni wakiendelea kutafutwa ili kufunguliwa mashtaka na kumkamata bibi harusi.

“Afisa wa uchunguzi amekamatwa. Wengine wako mbioni,” Bw Enanga alinukuliwa akisema.

 Inadaiwa mwanamke huyo kwa jina Christine Natuhera alikuwa ametoroka na kiasi cha shilingi milioni 8 za Uganda sawa na shilingi 240000 za Kenya kutoka taasis moja ya kifedha alikokuwa akihudumu kama mfanyikazi.

Msemaji huyo wa polisi alifichua kwamba awali kesi wa Natuhera kutoroka na fedha ilikuwa imeripotiwa mwendesha mashtaka wa umma ambaye aliamuru ifutiliwe mbali kwa vile ilikuwa inaonekana ya madai ya kawaida na kusema polisi hao watashtakiwa kwa vile walifanya maamuzi mabovu ya kuenda kumkamata mwanamke huyo licha ya kesi yake kuamriwa ifutwe.

"Kukamatwa hakukuidhinishwa na mimi, hakukuidhinishwa na DPC, au OC-CID. Huu ulikuwa ni mpango tu na mlalamishi na maafisa waliofanya makosa kwenda kumwaibisha bibi harusi,” akasema.

Mwanamke huyo baada ya kukamatwa Jumamosi katika harusi yake, aliachiliwa Jumapili baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rwizi kuamrisha kuachiliwa kwake mara moja bila shruti la aina yoyote ile.