"Tuko sawa" DJ Mo hatimaye avunja kimya kuhusu tetesi za kuachwa na Size 8

Wikendi tetesi zilichimbuka zikidai kuwa Size 8 aligura ndoa yao pamoja na watoto wao.

Muhtasari

•Wikendi ripoti nyingi zilisambaa mitandaoni zikidai kuwa mkewe Mo, Size 8 aligura ndoa yao pamoja na watoto wao na kuhamia kwingine.

•"Eeh, yuko!" Alisema kabla ya kumaliza mazungumzo ghafla, dokezo kuwa hakuwa tayari kuzungumzia mada hiyo zaidi.

Image: INSTAGRAM// DJ MO

Mcheza santuri mashuhuri Samuel Muraya almaarufu DJ Mo amezungumza kuhusu hali ya ndoa huku kukiwa na tetesi kuwa imesambaratika.

Wikendi ripoti nyingi zilisambaa mitandaoni zikidai kuwa mkewe Mo, Size 8 aligura ndoa yao pamoja na watoto wao na kuhamia kwingine.

Akizungumza na stesheni moja ya redio ya hapa nchini, Mo hata hivyo alipuuzilia madai ya kuvunjika kwa ndoa yake na kusisitiza kuwa iko imara

"Tuko sawa, tuko sawa, tuko sawa sisi," Mo alisema.

Alipoulizwa aliko Size 8, mcheza santuri huyo mwenye uzoefu mkubwa alidai kuwa bado hajaondoka nyumbani kwao.

"Eeh, yuko!" Alisema kabla ya kumaliza mazungumzo ghafla, dokezo kuwa hakuwa tayari kuzungumzia mada hiyo zaidi.

Siku chache zilizopita ripoti kadhaa zilichimbuka zikisema kuwa kuna matatizo katika familia ya Muraya.

Ilidaiwa kuwa mwimbaji na mchungaji, Linet Munyali almaarufu Size 8, haishi tena na mumewe DJ Mo kwenye nyumba yao ya ndoa.

Habari zilizofichuliwa na Mpasho.co.ke zilisema mama huyo wa watoto wawili alidaiwa kubeba vitu vyake na kwenda kuishi kwingine bila mumewe DJ Mo kutokana na migogoro ya kinyumbani.

Iliripotiwa kuwa Size 8 alimuacha Mo siku kadhaa zilizopita na kuwabeba watoto wao wawili. Juhudi za marafiki na familia kuwapatanisha wawili hao hazikuzaa matunda kwani Size 8 alikuwa amemkasirikia sana mumewe.

Vyanzo vya habari vilisema mwimbaji huyo aliwaomba marafiki na wanafamilia waliojaribu kuwapatanisha kumpa muda wa kufikiria kuhusu ndoa yao.

Walipotafutwa kwa njia ya simu ili kueleza hali halisi, wanandoa hao ambao wamekuwa pamoja kwa takriban mwongo mmoja hawakupatikana.

DJ Mo ambaye alisita kuzungumzia suala hilo alituomba tumpigie simu mkewe. Ujumbe na simu kwa Size 8 hazikujibiwa wakati wa kuenda hewani.

Kwenye Instagram, Wawili hao wame-unfollow kila mmoja.

Hii sio mara ya kwanza kwa wanandoa mashuhuri kuwa kwenye jicho la dhoruba.

Mwaka wa 2020, aliyedaiwa kuwa mchepuko wa DJ Mo alifichua mazungumzo na matukio yake ya karibu na mcheza santuri huyo kwa mwanablogu Edgar Obare, zikiwemo picha za DJ Mo akiwa uchi.

Wanandoa hao walifanya amani kwenye kipindi chao  'Dining with the Murayas' baada ya kile walichokiita 'Wiki ya masaibu'

"Sikutaka jambo hili limvunje au kumwangamiza au chochote shetani alitaka kufanya," Size 8 alieleza.