"Unatoka uachie nani nyumba na Range Rover?" Terence amdhihaki Size kwa kumuacha DJ Mo

Terence amemfanyia mzaha Size 8 kwa kitendo chake cha kugura ndoa yake kwa muda

Muhtasari

•Mchekeshaji huyo alimkaribisha tena  Size 8 nyumbani kwake na kumhoji mahali  alikokuwa akienda alipogura ndoa yake.

•Size 8 aliyacheka maneno ya mchekeshaji huyo na kueleza kujivunia kwake kumfanya mumewe awe na wasiwasi.

Terence Creative, Milly Chebby, The Wajesus, The Murayas wakutana
Image: INSTAGRAM// SIZE 8

Mchekeshaji Terence Creative amemfanyia mzaha Size 8 kwa kitendo chake cha kugura ndoa yake kwa muda siku kadhaa zilizopita.

Wasanii hao wawili walikutana jijini Nairobi kabla ya kuelekea kaunti ya Nakuru kwa ziara ya kikzai na kujiburudisha.

Katika video ambayo Terence alipakia kwenye Instagram, mchekeshaji huyo alimkaribisha tena  Size 8 nyumbani kwake na kumhoji alikokuwa akienda.

"Ni vizuri kurudi. Ulitetemesha mzee. Unatoka unaenda wapi uachie nani nyumba na Range Rover?" Terence alimwambia Size 8.

Size 8 kwa upande wake aliyacheka maneno ya mchekeshaji huyo na kueleza kujivunia kwake kumfanya mumewe awe na wasiwasi.

Terence alizidi kukejeli suala hilo huku  akimwambia mwimbaji huyo  kuwa pia yeye alikuwa ametoroka nyumbani kwake.

"Ni vizuri kurudi. Karibu nyumbani. Hata hivyo sisi bado tuko. Ata mimi nilikuwa nimetoka siku ingine," Alimwambia Size 8.

Wasanii wengine waliokuwa katika mkutano huo ni pamoja na DJ Mo, Kabi Wajesus, Milly Wajesus na Milly Chebby.

Wikendi iliyopika ripoti zilisambaa kuwa Size 8 alikuwa amegura ndoa yake na kuondoka pamoja na watoto wao.

Siku ya Jumatano mwimbaji huyo wa nyimbo za injili ambaye pia ni mhubiri alithibitisha kwamba alikuwa amemuacha mumewe.

Mama huyo wa watoto wawili aliweka wazi kuwa alikuwa amegura ndoa yake  baada ya mumewe  DJ Mo kumkosea vibaya.

"Ndio nilitoroka. Nilikuwa nimemkasirikia sana DJ Mo. Alinikosea. Nilihitaji tu nafasi yangu niweze kupumua na kuongea na Mungu kwa kuwa naamini nikiwa na hasira na tuko kwa nyumba moja tutaongeleshana vibaya na kufanyiana vibaya," Size 8 alisema huku akiwa amesimama sako kwa bako na mumewe.

Alidokeza kuwa kosa ambalo DJ Mo alimfanyia hadi kufanya atoroke ni kubwa, jambo ambalo mcheza santuri huyo alikiri.

"Ndio nilikosea, na nilisema pole," Mo alisema.

Size 8 alifichua kuwa watumishi wa Mungu na watu wengine wa karibu waliwasaidia kupatana na kusuluhisha mzozo wao.

"Tulifikia hitimisho na ufahamu wa kibiblia na sasa tumepatanishwa tena kwenye ndoa kwa sababu ya neema na rehema za Mungu," Alisema.

Aidha alifichua kuwa kipindi alichokuwa amekimbia ndoa yake na kuwabeba watoto wao Ladasha Wambui na Samue Muraya Jr, wawili hao walitamani sana kurudi nyumbani na hata kumuuliza ingefanyika lini.