Mungu ametenda-Ujumbe wa mkewe Rais mteule Rachel Ruto kwa mumewe

Rachel alipongeza ushindi wa hivi punde wa Ruto muda mfupi baada ya Mahakama ya upeo kutoa uamuzi wake.

Muhtasari
  • Mke wa rais mteule Mama Rachel Ruto ameandika ujumbe mzito kwa mumewe William Ruto ambaye uchaguzi wake uliidhinishwa na Mahakama ya upeo
Image: RACHEL RUTO/TWITTER

Mke wa rais mteule Mama Rachel Ruto ameandika ujumbe mzito kwa mumewe William Ruto ambaye uchaguzi wake uliidhinishwa na Mahakama ya upeo.

Rachel alipongeza ushindi wa hivi punde wa Ruto muda mfupi baada ya Mahakama ya upeo kutoa uamuzi wake.

“Hongera Bill mpenzi wangu. Mungu amefanya. Ninajivunia wewe! Akupe neema na hekima ya kuiongoza Kenya katika ukuu! Ulizaliwa na ulikusudiwa kwa hili!” alisema.

Aliendelea kunukuu andiko kutoka katika Biblia; Waebrania 10:23 inayosema,

"Na tushike kwa nguvu bila kuyumbayumba kwa tumaini tunalothibitisha kwamba Mungu anaweza kuaminiwa kutimiza ahadi yake."

Mke wa rais anayekuja pia aliongoza maombi katika makazi ya Naibu Rais huko Karen, ambapo watakuwa wakihama katika wiki zijazo.

Mahakama ya upeo imetangaza kwamba matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2022 yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati yameidhinishwa.

Chebukati alikuwa amemtangaza Ruto kuwa rais mteule baada ya kupata kura 7,176,141 (50.49%) dhidi ya kura 6,942,930 (48.85%) za mgombea urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga.