Serikali itenge nafasi za mwakilishi wa wazee bungeni - Fred Machokaa

Alisema wazee wananyimwa bima ya matibabu kwa sababu hawana watetezi bungeni.

Muhtasari

• "Lazima tupate wawakilishi wa kushughulikia mambo ya wazee hapa nchini Kenya kwa sababu wazee wamechezwa mbaya mbovu,” Machoka alisema.

 

Mtangazaji mkongwe Fred Obachi Machokaa
Mtangazaji mkongwe Fred Obachi Machokaa
Image: Facebook

Mtangazaji mkongwe wa vipindi vya nyimbo za Lingala na Rumba Fred Machoka amtoa wito kwa serikali kutenga nafasi za mwakilishi wa wazee bungeni.

Akizungumza kwenye kituo cha redio, Obachi Machoka alizua mzaha kwamba hilo linafaa kuzingatiwa na serikali ijayo ya rais William Ruto kwa kile alisema kwamba bungeni kuna wawakilishi wa vijana, kuna wawakilishi wa watu wenye ulemavu, kuna wawakilishi wa makundi ya kina mama ila hakujawahi kuwa viongozi wa kuwakilisha maslahi ya wazee.

“Mimi nazungumza tena, lazima wazee wapate mwakilishi bungeni. Kwa sababu hivi sasa tuko na wawakilishi wa vijana, tuko na wawakilishi wa wanawake na lazima tupate wawakilishi wa kushughulikia mambo ya wazee hapa nchini Kenya kwa sababu wazee wamechezwa mbaya mbovu,” Machoka alisema.

Mtangazaji huyo ambaye ni mzee na alionekana kuzungumza kwa niaba ya wazee alisema hata kampuni za kutoa bima siku hizi haziwezi kupatia wazee bima ya matibabu kwa sababu tu ya uzee wao.

“Yaani mtu unataka upewe bima unaambiwa huwezi kupewa kwa sababu wewe ni mzee, huo ni ukichaa wa aina gani? Ati wewe ni mzee. Sasa wanataka ufe? Hicho ndicho wanakitaka? Hatuwezi kubali hilo liendelee kufanyika kwa nchi ambayo imekuwa huru kwa takribani miaka 60,” Machoka alifoka kwa ukali.

Kulingana na Machoka, hali hiyo hujitokeza kwa sababu nchi haina wazee bungeni kutetea haki za wakongwe kupata bima ya matibabu.