(+videos) Njugush aigiza jinsi Ruto atatiririkwa na machozi wakati wa kuapishwa

Njugush alikuwa akiigiza kwa sauti ya rais mteule William Ruto.

Muhtasari

• Kila baada ya kujaribu kuinua biblia, Njugush anaigiza kama anajawa na hisia na kukatisha kuapa kwake huku akiitisha hanchifu zaidi za kupangusa machozi.

Mchekeshaji Blessed Njugush ameachia video ya kuchekesha kwenye ukurasa wake wa Instagram akielezea ni kwa nini kuapishwa kwa rais mteule William Ruto kutachukua muda mrefu Jumanne wiki kesho.

Katika video hiyo, Njugush ambaye anaiga Ruto kwa sauti na hata kuvalia anaonekana akiinua biblia kula Yamini ya kuwatumikia Wakenya kama rais wa tano.

Kila baada ya kujaribu kuinua biblia, Njugush anaigiza kama anajawa na hisia na kukatisha kuapa kwake huku akiitisha hanchifu zaidi za kupangusa machozi.

Katika igizo hilo, Njugush alionekana kuigiza hisia za William Ruto ambaye wiki chache kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9 alionekana akizidiwa na hisia wakati wa ibada iliyofanyika katika makazi ya naibu rais eneo la Karen Nairobi.

Ruto kwa mara kadhaa amekuwa akionekana kuzidiwa na hisia na kutokwa na machozi na wengi walikuwa wanasema ni kwa sababu amepitia changamoto nyingi kama naibu rais haswa baada ya Handshake iliyomfanya kutofautiana vikali na bosi wake Rais Uhuru Kenyatta.

Mshereheshaji wa hafla hiyo analitaja jina la rais na Njugush anaonekana kuwa na furaha ila pindi tu anapoinua Biblia juu kuapa, anazidiwa na hisia na kukatanisha kiapo hicho.

Njugush anasema kwamba kutokana na hisia za Ruto kuwa nyingi, hafla hiyo itachukua siku mbili ili kukamilika.

Mahakama ya juu ilipothibitisha ushindi wa Ruto mapema wiki hii, yeye, pamoja na mkewe na viongozi wengine wa Kenya Kwanza, walipiga magoti kuomba. Katika video hiyo yenye hisia, viongozi hao walianza kupiga makofi jaji mkuu Martha Koome alipoidhinisha ushindi wa Ruto, lakini Rais Mteule alipiga magoti mara moja, akainamisha kichwa chake na kuanza kusali.