(+video) Kioja JKIA mwanadada akimshambulia ajenti baada ya kurudi kutoka Saudia

"Ulituuza Saudi Arabia, ulikuwa unataka tufe!" mwanadada alifoka akimrukia wakala huyo.

Muhtasari

• Alieleza kwamba kwa miezi mitano, amekuwa akipitia mateso makali mpaka kunywa maji ya taka huko Uarabuni.

Mwanamke mmoja alizua kioja katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) baada ya kurudi kutoka Saudi Arabia alikoenda kufanya kazi kama mfanyikazi wa ndani.

Inasemekana kwamba mwanamke huyo alikuwa miongoni mwa wale walionusuriwa baada ya kuteta kuwa mazingira ya kufanya kazi katika taifa hilo ya Mashariki ya kati hayakuwa mazuri kwake kabisa na kulazimika kuukatisha mkataba wake ili kurejea nyumbani Kenya.

Kioja chenyewe kilifuatishwa na vurumai alipofika JKIA na kumuona wakala yule ambaye aliwakusanya wanadada na kuwatuma Saudia kufanya kazi.

Katika video ambayo imesambazwa mitandaoni na Wakenya mbali mbali, mwanadada huyo anaonekana akizungumza na waandishi wa habari na ghafla kukatisha mahojiano anapomuona ajenti yule aliyemwezesha Kwenda Uarabuni.

Anamrukia ghafla kwa hasira huku akifoka kuwa anataka kumrarua kwa kile alisikika akiteta ajenti huyo aliwauza Uarabuni pasi na kufuatilia mahusiano yao na waajiri ambao aliwaunganisha nao.

Kwa bahati nzuri kulikuweko na watu ambao walijaribu kumzuia na kumtuliza mwanadada huyo aliyejawa na hasira zilizopitiliza za Samaki mkizi. Hata baada ya kuzuiliwa, mwanadada anajitahidi kujinasua mikononi mwa watu ili kumkaba ajenti huyo mwanamke ambaye amevalia baibui.

“Huyu mwanamke ndiye alituuza Saudi Arabia, alikuwa anataka tufe, niache nimshike, niache,” mwanadada wa watu anafoka kwa hasira na kujinasua mikononi mwa watu kabla ya kumkaba vikali ajenti huyo.

Polisi anafika kutuliza hali ambapo ajenti anachukuliwa na watu wa karibu naye huku mwanadada akijieleza kwa polisi kwamba alikuwa anataka kumtia bisu la koromelo angalau hasira zake zipungue.

“Wewe ulituuza Saudia, na wewe ni mwanamke kama mimi, ulikuwa unafikiria mimi sikuzaliwa na mtu? Halafu unakuja kuniona hapa. Enda usaidie watoto wa watu wanaoteseka huko Saudia kwanza, hiyo ofisi yako lazima ifungwe. Si eti unakuja kuniona hapa na niliumia,” mwanadada huyo anatema moto.

Katika video hiyo, mwanadada huyo anaeleza jinsi alivyopitia mateso mikononi mwa mwajiri Mwarabu ambapo anadokeza kwamba miezi mitano kwake ilikuwa kama karne kadhaa. Alikuwa akinywa maji ya taka.