"Mtoto sio kazi!" Mulamwah amkaripia Sonnie, amtaka kurahisisha uzazi wenza

Mchekeshaji huyo alieleza hamu yake ya kukutana na bintiye na kushiriki mazungumzo katika siku za usoni.

Muhtasari

•Keilah Oyando, ambaye alizaliwa katika kipindi ambacho wazazi wake walikuwa wakitengana alitimiza mwaka mmoja.

•Mulamwah alidokeza kuwa haijakuwa rahisi kwake na Sonnie kuwa wazazi wenza na kumsihi  kuifanya iwe rahisi.

Carrol Sonnie na aliyekuwa mpenzi wake Mulamwah
Image: HISANI

Jumamosi, Septemba 17, mchekeshaji Mulamwah na aliyekuwa mpenzi wake Caroline Muthoni walisherehekea siku ya kuzaliwa ya binti yao.

Keilah Oyando, ambaye alizaliwa katika kipindi ambacho wazazi wake walikuwa wakitengana alitimiza mwaka mmoja.

Huku akimsherehekea bintiye kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Mulamwah alimtakia  baraka tele maishani na kueleza hamu yake ya kukutana naye  na kushiriki mazungumzo katika siku za usoni.

"Nakutakia miaka mingi zaidi ya ukuaji na afya njema. Siku moja tutakutana na tuzungumze pindi utakapokuwa na akili yako mwenyewe," alisema.

Mchekeshaji huyo ambaye kitaaluma ni muuguzi pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Sonnie kwa kuendelea kumlea binti yao vizuri.

Hata hivyo alidokeza kuwa haijakuwa rahisi kwao kuwa wazazi wenza na kumsihi muigizaji huyo kuifanya iwe rahisi.

"Tusimtumie mtoto kama chambo ili kupata likes kwenye mitandao ya kijamii kupenda mitandao ya kijamii, uthibitisho na kupata faida ya pesa. Mtoi sio kazi," Mulamwah alimwambia aliyekuwa mpenziwe.

"Heri ya siku ya kuzaliwa malkia, tunakungoja Kitale bado. Dada yako mdogo amekusalimia pia. HBD Kalamwah Keilah Oyando. Baraka," alimwandikia bintiye.

Kwa upande wake Sonnie alibainisha kuwa ni furaha kubwa kwake kumuona bintiye akipiga hatua maishani.

"Kukuona ukikua kila siku imekuwa nyakati zangu bora zaidi. Kwa kweli siwezi kungoja kukuona ukizeeka na kuwa Mtoto anayemcha Mungu.. Ninakupenda sana. Heri ya kuzaliwa mpenzi wangu," Sonnie alimwandikia bintiye.

Jumamosi muigizaji huyo alimpeleka bintiye kusherehekea siku ya kuzaliwa mjini Mombasa kwa ufadhili wa kampuni moja ya usafiri.