Video ya mtoto yatima akishukuru baada ya kupakuliwa chakula yaliza wengi

Mtoto huyo alipakuliwa na kabla hajaanza kula alichukua muda kiasi na kushukuru kwa kusujudu

Muhtasari

• “Mungu awabariki wote hasa huyu dogo mwenye moyo wa shukrani,” Loritt aliandika.

Mtoto mmoja mdogo ambaye anaishi katika boma la watoto mayatima aliwaliza wengi kwenye mtandao wa Instagram baada ya klipu kusambazwa akionekana kusujudu kwa kupokea chakula.

Mtoto huyo mdogo mwenye umri wa chini ya miaka 5 alionekana kupanga laini kupakuliwa chakula na wahisani wema waliotembelea boma hilo na baada ya kupakuliwa, aliinama kama kusujudu vile kabla ya kuondoka kutafuta sehemu ya kukaa ili kula.

Kama haitoshi, baada ya mtoto huyo kufika sehemu ya kuketi, aliweka chakula kando na kuchukua sekunde kadhaa ambapo alionekana kama anapiga sala kabla ya kuanza mashambulizi ya kutuliza njaa.

Video hiyo ilipakiwa intagram ya Yahweh Children Ministries na watu wengi walilizwa machozi ya huruma na furaha kwa kitendo cha mtoto huyo mdogo kuonesha shukrani kwa kupata chakula, wali kwa maharagwe.

Haya hapa ni baadhi ya maoni kutoka kwa watu walioona video hiyo.

“Mungu awabariki wote hasa huyu dogo mwenye moyo wa shukrani,” Loritt aliandika.

“Nimejipata nikilia 😭 bwana awabariki nyote kwa matendo mema mnayofanya,” Mercy Cheetham aliandika kwa hisia kali.

“Na hata alisema neema 😢Mungu awabariki wote na wale wanaotoa milo yao 🙏” Savage Toa alisema.

Wengine walitaka kujua boma hili la kuwalea watoto wasio na wazazi lipo wapi mradi wakatembee kule kutoa msaada wao kutokana na kuvutiwa na kitendo cha unyenyekevu cha yule dogo.

Baadhi walisema kuna fadhila nyingi tu mtu anaweza kujizolea hapa duniani kwa kutoa msaada kwa watoto kama hao wenye shukrani tele ila wakaonesha kushangazwa kwao ni kwa nini wanasayansi wanatumia fedha nyingi kusafiri angali kufanya utafiti ili wapate sifa.

“Na tunatumia mabilioni kwenda angani kutafuta vithibitisho vya maisha....si ni kichaa?”