"Nataka afike juu kama Diamond!" Khadija Kopa afichua anayemwandikia nyimbo bintiye Zuchu

Mamake Zuchu alisema bintiye hupokea mawaidha ya muziki kutoka kwa wenzake katika WCB.

Muhtasari

•"Wasanii wengi hawajui kuandika, wanasubiri wapewe nyimbo waweze kufanya lakini hawaandiki wenyewe," Kopa alisema.

•Alisema kuwa bintiye yuko kwenye kiwango cha juu cha uimbaji na kumtakia mafanikio ziadi katika kazi yake ya usanii.

Khadija Kopa na binti yake Zuchu
Image: HISANI

Mwimbaji mkongwe wa nyimbo za taarab Khadija Kopa ameweka wazi kuwa binti yake Zuchu huandika nyimbo zake mwenyewe.

Katika mahojiana na Mbengo TV, Bi Kopa alibainisha kuwa waandishi wengi wa kike huwa wanaandikiwa nyimbo lakini akasisitiza kuwa binti yake hajawahi kuomba usaidizi katika utunzi wa nyimbo zake.

"Wasanii wengi hawajui kuandika, wanasubiri wapewe nyimbo waweze kufanya lakini hawaandiki wenyewe," alisema.

Aliongeza, "Zuchu ni hodari. Hata wasanii wenzie wa kiume wanamwambia kuwa anajitahidi. Nyimbo zile zote anajiandikia mwenyewe, haandikiwi na mtu. Hakuna mtu ambaye anapitisha kalamu yake," 

Malkia huyo wa Mipasho hata hivyo alidokeza kuwa Zuchu hupokea mawaidha ya muziki kutoka kwa wenzake katika WCB.

Alisema kuwa bintiye yuko kwenye kiwango cha juu cha uimbaji na kumtakia mafanikio ziadi katika kazi yake ya usanii.

"Yuko vizuri. Simfananishi na yeyote, nataka aende zaidi afanane na kina Beyonce. Nataka aende afike juu kama walikofika kina Diamond," alisema.

Aidha aliwasuta wasanii wenza wa Zuchu ambao wamekuwa wakimkosoa baada ya kujigamba kuhusu ubabe wake katika muziki

Siku kadhaa zilizopita Zuchu ambaye kwa sasa anaaminika kuwa miongoni kwa wasanii bora wa kike nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki alitoa ombi kutoshindanishwa tena na wasanii wenzake wa kike.

Staa huyo wa Bongo kutoka Zanzibar alidai kuwa ligi yake ni ya wanaume na kutaka kushindanishwa nao tu kuendelea.

“Kwa uandishi wangu yafaa kuwekwa kwenye ligi za wanaume, wadada wenzangu nitawaonea tu kwa heshima!” alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Pia alijigamba kuwa hata anaweza kumwandikia wimbo msanii wa kiume ya kusiwe na yeyote atakayegundua.

“Naachilia ngoma mbili mwezi huu,” alitangaza.

Zuchu aliwashukuru wazazi wake, Bi Khadija Kopa na Bw Othman Soud  kwa kuwezesha na kukuza  kipaji chake cha usanii.