"Ndio nimesota!" Juliani aeleza kwa nini anakabiliwa na changamoto za kifedha

Alifichua kuwa changamoto zinazomkabili zimesababisha yeye kukosa muda wa kuwa mwanawe.

Muhtasari

•Rapa huyo alidokeza kwamba hata alichukua madeni kadhaa katika juhudi za kukamilisha baadhi ya miradi yake.

•"Pesa ambazo nimekuwa nikiwekeza miaka mitano iliyopita hazijaleta faida bado," alisema.

Image: INSTAGRAM// JULIANI

Mwimbaji wa nyimbo za kufoka Julius Owino almaarufu Juliani amekiri kwamba anakabiliwa na changamoto za kifedha.

Katika taarifa ya video ambayo alitoa Jumatano alasiri kupitia mitandao ya kijamii, Juliani hata hivyo alibainisha kuwa bado hajafilisika.

Alieleza kuwa changamoto zinazomkabili zimetokana na kiasi kikubwa cha fedha ambacho ametumia kwenye miradi yake katika siku za nyuma.

"Katika miaka mitatu iliyopita nimekuwa nikiweka pesa zangu kwa kila kitu nilichofanya. Sina wafadhili, sina wawekezaji, sina chochote. Nimeweka pesa zangu kidogo kwa ajili ya hayo," alisema katika video aliyopakia Twitter.

Rapa huyo alidokeza kwamba hata alichukua madeni kadhaa katika juhudi za kukamilisha baadhi ya miradi yake.

Aidha alifichua kuwa changamoto za kifedha zinazomkabili kwa sasa zimesababisha yeye kukosa muda wa kuwa mwanawe huku akimshukuru mkewe na mzazi mwenzake Lilian Nganga kwa kumuelewa.

"Siwezi kupata muda na mwanangu sasa kwa sababu nahangaika huku na kule nikijaribu kulipa madeni niliyochukua ili kutimiza mambo kadhaa ambayo nilijiahidi kutimiza. Namshukuru sana mama (Lilian) kwa kuelewa ninachojaribu kufanya," alisema.

Juliani hata hivyo alibainisha kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto za kifedha bado hajafilisika kwani angali anaweza kukidhi mahitaji muhimu.

"Mkiniona nikihangaika sifanyi, sifanyi hayo yote kwa ajili yangu mwenyewe. Niko sawa , kuna paa juu yangu naweza kujilisha lakini niko na ndoto zangu," alisema.

Alitaja baadhi ya maazimio yake kuwa kutengeza nafasi 10,000 za kazi, kupatia wasanii mikopo na kuachilia muziki zaidi. Alisema kuwa amejipatia miaka 10 kutimiza ndoto aliyo nayo kwa jamii yake.

"Pesa ambazo nimekuwa nikiwekeza miaka mitano iliyopita hazijaleta faida bado," alisema.

Pia alieleza kusikitishwa kwake na watu wanaofanya mzaha kuhusu hali yake ya sasa na kuwaomba wakome kuendelea.

Hapo awali msanii huyo alichapisha ujumbe akiomba kusaidiwa kulea mtoto wake na mkewe  Lilian Nganga.

Katika chapisho lake la utani Jumatano asubuhi, Juliani alidai kuwa amefilisika na kuwaomba Wakenya kumchangia pesa za kununua nepi  za mwanawe mdogo kupitia Mpesa. Alijitambulisha kama rapa  na mjasiriamali anayeteseka.

"Wase! Nikubaya niko BROKE! mtoi anahitaji pampers.. Tafadhali tumeni mpesa. Lipa na M-PESA 784577, Akaunti- Juliani," aliandika.

Alimalizia "Chochote unaweza kitasaidia. Ni wenu, niRapa/mjasiriamali anayeteseka,"

Ujumbe huo wa utani wa rapa huyo ulifuatia uvumi na habari nyingi za uwongo kuhusu uwezo wake wa kifedha ambazo zimekuwa zikichapishwa kwenye mitandao ya kijamii katika siku za hivi majuzi.