(+video) Wafanyibiashara washiriki mchezo wa kitoto wa kuruka kamba sokoni

Kina mama hao walionekana wakiruka kamba kwa zamu huku wakisubiria wateja katika soko la Kutus Kirinyaga

Muhtasari

• Video hiyo ilianza kwa kuwaonyesha wanawake wawili wakiwa katikati tayari kwa kuruka kamba iliyotengenezwa kwa vipande vya nguo vilivyofungwa pamoja.

Katika dunia ya sasa na utandawazi, mtu yeyote yule hawezi kosa sababu ya kuwa na furaha kutokana na matukio ya mitandaoni, labda uwe huna bando.

Kila siku ya Mungu matukio mbali mbali ya kufurahisha na mengine ya kuchukiza hufanyika katika sehemu mbali mbali kote duniani, na wengi hupata kuyajua pindi tu yanapopakiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa mfano kuna video moja imepakiwa kwenye mtandao wa Facebook ikiwaonesha wanawake wafanyibiashara wakishiriki mchezo wa kuruka Kamba sokoni huku wakiwasubiri wateja.

Video hiyo iliarifiwa kuchukuliwa katika soko la Kutus kaunti ya Kirinyaga iliwaonesha makumi ya wanawake waliokomaa kiumri kutokana na muonekano wao. Kina mama hao wanaonekana kwa furaha wakishiriki mchezo wa kitoto wa kuruka Kamba kwa zamu.

Wakenya wengi walivutiwa na video hiyo, huku wengi wakisema ilikuwa bora na njia ya kujiachia na kuwa na wakati mzuri, kwani si kila mara mtu unafaa kuchukulia maisha kwa uzito vile.

Video hiyo ilianza kwa kuwaonyesha wanawake wawili wakiwa katikati tayari kwa kuruka kamba iliyotengenezwa kwa vipande vya nguo vilivyofungwa pamoja.

Kina mama hao wawili waanzilishi wa mchezo huo Walifanikiwa kuruka mara mbili kabla ya mmoja wao kukanyaga kamba. Baada ya hapo, alichukua changamoto hiyo peke yake na akairuka kwa furaha kwa muda.

Kikundi kingine cha wanawake kiliingia kwenye uangalizi, huku mmoja aliyevalia sweta jekundu akirukaruka kwa muda kwa muda. Kikundi kilionekana kufurahia mchezo huo, ukumbusho wa miaka yao ya ujana. Munene, mpiga picha, alinukuu klipu hiyo kwa kuwataka watu kufurahia maisha kikamilifu.