(+video) Azua fujo ndani ya benki kwa kutotumiwa meseji ya 'birthday', ataka kufunga akunti yake

Mwanaume huyo alielekea kwenye benki na kuteta kwa benki hiyo kukosa kumtumia meseji ya kumtakia heri njema siku yake ya kuzaliwa.

Muhtasari

• Alisimama hapo akitaka benki hiyo kumtumia meseji hiyo au aifunge akaunti yake.

• Wateja wenzake walimuimbia wimbo wa kumtakia heri njema ya kuzaliwa na hapo ndipo alitulia na kuondoka zake.

Tamaduni za kuficha fedha chini ya godoro ama kwenye kibubu ndani ya nyumba zilipitwa na wakati huku watu wengi wakikumbatia mifumo ya benki kuweka pesa zao.

Ukiuliza watu wengi umuhimu wa benki katika maisha yao, bila shaka hawatakosea kukuambia tena kwa mikogo kwamba hizo ni taasisi za kuhakikisha usalama wa fedha za watu.

Lakini kwa jamaa mmoja, benki ina majukumu mengine kando na kuhakikisha usalama wa pesa za watu!

Jamaa huyo alionekana kwenye klipu moja akizua mfarakano mkali katika benki moja kwa kutotumia ujumbe wa heri njema ya siku yake ya kuzaliwa na benki hiyo ambayo amefungua akaunti ya kuweka pesa zake.

Katika klipu huyo, bwana mwenye midevu yake anaonekana akizua vikali kwa mfanyikazi wa benki kwa kile anasema kuwa siku yake ya kuzaliwa ilikuwa siku moja nyuma na hakupokea meseji ya kumtakia heri njema kutoka kwa benki hiyo kama ambavyo benki zingine hufanya kwa wateja wao.

Alijieleza kwa watu waliojongea karibu kusikilizia ugomvi huo na kuwaambia kwamba alipokea meseji za heri njema kutoka kwa benki zingine ambazo amefungua akaunti nazo ila hii ndio tu haikumtambua na kwake yeye alitafsiri kitendo kuwa hathaminiwi kama mteja.

Watu walijaribu kumtuliza bila kufua dafu na akasisitiza kwamba haondoki hapo kabla hajapata mwafaka wa suala hilo.

Alitaka benki hiyo kuchagua moja kati ya kumtumia meseji hiyo ya kumtakia heri njema ya siku ya kuzaliwa mara hiyo kabla hajaondoka au aifunge akaunti yake na kuvunja uswahiba wake na benki mara moja.

Huku bwana huyo akiendelea kuzua, wateja wenzake waliokuwa wanasubiri kuhudumiwa walimshtukizia kwa wimbo wa heri njema ya kuzaliwa na kidogo sura ya mwanaume huyo ilionekana kulainika na tabasamu likachomoza ghafla usoni mwake, kabla ya kuwashukuru wateja wenzake na kuondoka zake safari hii akionekana kuridhika.