"Sikutaka stori ya mwanamke!" Juliani afunguka jinsi alivyokutana na mkewe Lilian Ng'ang'a

Rapa huyo amekana madai kuwa aliiba mke wa gavana wa zamani wa Machakos, Alfed Mutua.

Muhtasari

•Juliani alisema alikutana na mpenzi huyo wa zamani wa aliyekuwa gavana wa Machakos Alfred Mutua mwaka jana bila mpango

•Rapa huyo alifichua kuwa wakati huo alikuwa akijiangazia mwenyewe na hakutaka chochote kuhusu wanawake.

Lilian Ng'ang'a na Juliani
Image: INSTAGRAM// JULIANI

Mwimbaji Julius Owino almaarufu Juliani amesema alikuwa amekata tamaa ya kuchumbiana wakati alipokutana na mke wake Lilian Ng'ang'a.

Akiwa kwenye mahojiano katika kituo kimoja cha redio cha hapa nchini siku ya Jumatano, rapa huyo alifichua kuwa wakati huo alikuwa akijiangazia mwenyewe na hakutaka chochote kuhusu wanawake

"Nilikuwa celibate wakati huo ata sikutaka stori ya manzi ju nilikuwa mahali poa sana. Lakini vitu vilichukua mkondo tu vile inafaa," alisimulia.

Juliani alisema alikutana na mpenzi huyo wa zamani wa aliyekuwa gavana wa Machakos Alfred Mutua mwaka jana bila mpango.

Alibainisha kuwa hakuwa akitafuta mchumba wakati huo ila baada ya kuwa marafiki kwa muda wakajipata kwenye mahusiano.

"Baadae aliniambia kusema kweli hivi ndio kuko, mimi siko hapo. Mimi nilisema sikuwa najua nilidhani sisi ni mabeshte tu," alisema.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za kufoka alitupilia mbali madai kuwa aliiba mke wa waziri aliyependekezwa wa masuala ya kigeni, Alfed Mutua.

Alisema hakujua kilichokuwa kinaendelea katika maisha ya Lilian walipokutana na alikuja kujua kuhusu kuvunjika kwa ndoa yake na Mutua baadae.

"Huwezi kunyang'anya jamaa mtu wake. Haifanyiki hivyo. Watu wanapenda madai kama hayo kwa hivyo wanaegemea upande ambao sio," alisema.

Juliani na Lilian walitangaza mahusiano yao Septemba mwaka jana, wiki chache tu baada ya Alfred Mutua na Mama Machakos huyo wa zamani kutangaza kutengana kwao baada ya kuwa pamoja kwa takriban mwongo mmoja.

Katika mahojiano ya awali juliani aliweka wazi kuwa hakupanga kujitosa kwenye mahusiano na Bi Lillian, lakini mambo yalizidi kasi baada ya mama huyo wa mtoto mmoja kuchukua namba yake.

Mwaka mmoja baadaye, wawili hao ni wazazi wa mtoto wa kiume anayeitwa Utheri (mwanga).