Huru rasmi! Anerlisa Muigai hatimaye akamilisha talaka yake na Ben Pol

Baada yao kutengana mwaka jana, Ben Pol aliwasilisha talaka mahakamani.

Muhtasari

•Anerlisa amewashukuru mawakili wake kwa kuhakikisha kuwa mchakato wa talaka yake umekamilika.

"Rasmi Anerlisa na Ben si mume na mke tena, talaka imetolewa leo jioni ya saa tisa. Hongera," ujumbe mmoja ulisoma.

Ben Pol na Anerlisa Muigai
Image: HISANI

Ni rasmi kuwa mfanyabiashara wa Kenya  Anerlisa Muigai na mwimbaji wa R'n'b kutoka Tanzania Ben Pol sio mke na mume tena.

Anerlisa na Ben Pol walifunga ndoa Mei 2020 katika Kanisa Katoliki la St Gaspar huko Mbezi Beach, Tanzania lakini wakatengana mwaka jana. Baada ya kutengana, Ben aliwasilisha kesi ya talaka mahakamani.

Katika chapisho lake la hivi punde kwenye Instagram, Anerlisa ambaye ni binti wa seneta wa Nakuru Tabitha Karanja amefichua kuwa talaka yake na mwimbaji huyo wa Bongo hatimaye imekamilika.

Mridhi huyo wa Keroche amewashukuru mawakili wake kwa kuhakikisha kuwa mchakato wa talaka yake umekamilika.

"Niko huru rasmi. Haitakuwa sawa kutowatambua mawakili hawa wawili ambao walifanya kazi bila kuchoka kuhakikisha kwamba talaka inafanywa haraka na sio kusubiri kwa miaka. Hamza Jabir na Hosea Chamba, asanteni kwa kazi zenu na kwa kufanya kila kitu mlivyoombwa," alisema kwenye Instasori zake.

Aliendelea kufichua mazungumzo yake na mmoja wa mawakili wake kuthibitisha kuwa talaka hiyo imekamilika.

"Rasmi Anerlisa na Ben si mume na mke tena, talaka imetolewa leo jioni ya saa tisa. Hongera," ujumbe mmoja ulisoma.

Image: INSTAGRAM// ANERLISA MUIGAI

Ben aliwasilisha ombi la talaka mahakamani miezi kadhaa baada ya kutengana na mfanyibiashara huyo  kwa misingi ya tofauti zisizoweza kusuluhishwa na sababu zingine ambazo hazikuwekwa wazi.

Mapema mwaka huu staa huyo wa Bong akiwa katika mahojiano alisema ulikuwa mpango wa Mungu wao kwenda njia zao tofauti.

"Huwezi kubainisha kitu kimoja na kusema hiki ndicho kilichotokea. Ulimwengu ndio ulioturuhusu kwenda njia tofauti. Sote wawili. Naweza kusema ulikuwa mpango wa Mungu.” alisema katika mahojiano na Mpasho.

Ben ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Kenya aliweka wazi kuwa bado hajaoa tena licha ya mkewe wa zamani kuendelea na mtu mwingine.

“Bado sijaoa. Nimekuwa nikishughulika na kazi na kusafiri lakini sijui la kusema. Swali hilo linaweza lisiwasaidie watu lakini ndio sijaoa,” alisema.

Kabla ya kukutana na Anerlisa, Ben Pol alikuwa kwenye mahusiano na mama wa mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 6. Baada ya kuachana na Anerlisa, Ben Pol alitafuta ushauri nasaha na kujiangazia mwenyewe.