Ben Pol hatimaye avunja kimya kuhusu kukamilika kwa talaka yake na Anerlisa

Staa huyo wa Bongo RnB amesema alifikiwa na habari hizo kupitia mitandao.

Muhtasari

•Wiki iliyopita mfanyibiashara Anerlisa Muigai alitangaza kuwa mchakato wa talaka yake na Ben Pol umekamilika.

•Ben Pol amesema hajapata taarifa yoyote kuhusu kukamilika kwa talaka yao.

Ben Pol na Anerlisa Muigai
Image: HISANI

Staa wa Bongo RnB Ben Pol amepuuzilia mbali madai ya aliyekuwa mkewe, Anerlisa Muigai, kuwa talaka yao hatimaye imekamilika

Wiki jana binti huyo wa seneta wa Nakuru Tabitha Karanja alitangaza kuwa mchakato wa talaka yake na Ben umekamilika.

Mridhi huyo wa Keroche aliwashukuru mawakili wake kwa kuhakikisha kuwa mchakato wa talaka yake umekamilika.

"Niko huru rasmi. Haitakuwa sawa kutowatambua mawakili hawa wawili ambao walifanya kazi bila kuchoka kuhakikisha kwamba talaka inafanywa haraka na sio kusubiri kwa miaka. Hamza Jabir na Hosea Chamba, asanteni kwa kazi zenu na kwa kufanya kila kitu mlivyoombwa," alisema kwenye Instasori zake.

Siku chache baadae hata hivyo, Ben Pol amejitokeza kusema kuwa hajapata taarifa yoyote kuhusu kukamilika kwa talaka yao na kueleza kuwa hata yeye, kama vile wengi, alifikiwa na habari hizo kupitia mitandao.

"Mimi pia naona ripoti hizi mtandaoni. Sijafahamishwa rasmi au kwa njia isiyo rasmi. Sijui hayo mawasiliano aliyapata wapi maana hata mahakama niliyofungua kesi ya talaka haifahamu taarifa hizo," Ben Pol aliambia Nation

Mwimbaji huyo alibainisha kuwa kesi hiyo aliyowasilisha mwaka wa 2020 iko mahakamani na anasubiri matokeo yake.

Huku akieleza furaha yake kubwa kufuatia kukamilika kwa talaka, Bi Anerlisa pia alifichua mazungumzo yake ya WhatsApp kati yake na mmoja wa mawakili wake kuthibitisha kuwa talaka hiyo imekamilika.

"Rasmi Anerlisa na Ben si mume na mke tena, talaka imetolewa leo jioni ya saa tisa. Hongera," ujumbe mmoja ulisoma.

Ben aliwasilisha ombi la talaka mahakamani miezi kadhaa baada ya kutengana na mfanyibiashara huyo  kwa misingi ya tofauti zisizoweza kusuluhishwa na sababu zingine ambazo hazikuwekwa wazi.

Mapema mwaka huu staa huyo wa Bongo akiwa katika mahojiano alisema ulikuwa mpango wa Mungu wao kwenda njia zao tofauti.

"Huwezi kubainisha kitu kimoja na kusema hiki ndicho kilichotokea. Ulimwengu ndio ulioturuhusu kwenda njia tofauti. Sote wawili. Naweza kusema ulikuwa mpango wa Mungu.” alisema katika mahojiano na Mpasho.

Ben ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Kenya aliweka wazi kuwa bado hajaoa tena licha ya mkewe wa zamani kuendelea na mtu mwingine.

“Bado sijaoa. Nimekuwa nikishughulika na kazi na kusafiri lakini sijui la kusema. Swali hilo linaweza lisiwasaidie watu lakini ndio sijaoa,” alisema.

Kabla ya kukutana na Anerlisa, Ben Pol alikuwa kwenye mahusiano na mama wa mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 6. Baada ya kuachana na Anerlisa, Ben Pol alitafuta ushauri nasaha na kujiangazia mwenyewe