(+video) Mama aalika marafiki 40 kwa sherehe ya kuzaliwa kwake, wote wagoma kutokea

Wanamitandao walimuonea huruma mama huyo aliyekuwa akilia baada ya kuandaa chakula ambapo marafiki wake hawakutokea kusherehekea naye.

Muhtasari

• “Angalia kama aliweka tarehe sawa katika mialiko ile, haiwezekani watu zaidi ya 40 asitokee hata mmoja,” Mer alishauri.

Mwanamke mmoja alipatwa na mshtuko wa maisha yake baada ya kupanga tafrija la kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na kuwaalika marafiki zake kadhaa lakini hakuna rafiki hata mmoja aliyejitokeza mpaka jua lilipozama jioni kabisa.

Katika video ambayo sasa imesambaa kwenye mitandao ya kijamii utadhani moto wa jangwa la Sahara, mshereheshaji aliyekabidhiwa na jukumu la kufawidhi sherehe hiyo aliipakia na kueleza sikitiko la mama huyo ambaye alionekana amesawijika uso kutokana na kitendo cha marafiki zake kuupuzilia mbali mwaliko wa kusherehekea na yeye siku yake ya kuzaliwa.

Mshereheshaji huyo ambaye pia alikuwa mwanawe mama huyo aliandika kwa uchungu kuwa mama yake alitengeneza chakula na kusafisha nyumba nzima kwa hafla hiyo lakini marafiki zake wote wakakwepa kuhudhuria na kumwacha mama mtu katika hali ya mafikirio mengi, ashindwe cha kujijibu.

"Mama yangu alijiandalia sherehe ya kuzaliwa na kuwaalika zaidi ya watu 40. Ni saa kumi na moja jioni, hakuna aliyejitokeza na ilianza saa kumi jioni, ninalia. Alitengeneza chakula na kusafisha nyumba nzima pia.” kijana huyo aliandika kwenye video hiyo.

Katika video hiyo ambayo wimbo wa huzuni unasikika kwa mbali, maam mtu anaonekana akiwa analengwa na machozi, kitu ambacho kiliwauma baadhi ya watumizi wa Tiktok na wengine pia hawakukosa kuzua utani kwa hali hiyo.

“Ningalikuwapo karibu ningejitokeza kwa ajili yake tu, anastahili bora zaidi na anatia huruma mama wa watu,” mmoja kwa jina May aliandika.

“Hili linauma moyo wangu sana lakini amebarikiwa kuwa na wewe kijana wake,” mwingine alimtia moyo.

“Angalia kama aliweka tarehe sawa katika mialiko ile, haiwezekani watu zaidi ya 40 asitokee hata mmoja,” Mer alishauri.