"Unarisk!" Mulamwah amuonya mwanadada Mluhya aliyemmezea mate

Mchekeshaji huyo pia aliweka wazi kuwa kwa sasa hachumbiani na mtu yeyote.

Muhtasari

•Mwanadada mmoja kutoka nyumbani kwao Kitale alichukua hatua ya ujasiri na kumwomba mchekeshaji huyo amchukue kama mchumba wake.

•Mulamwah pia alionekana kupuuza maombi mengi ya kukutana kutoka kwa mashabiki wake.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah aliwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram siku ya Jumatano.

Katika kipindi hicho, mashabiki waliuliza maswali, wakatoa maoni, wakampongeza mchekeshaji huyo, wakatoa mapendekezo kwake na baadhi wakamkosoa.

Kama inavyotarajiwa, wanamitandao wengi walikuwa makini zaidi na maisha ya mahusiano ya baba huyo wa binti mmoja.

"Uko single?" shabiki mmoja aliuliza.

Katika jibu lake, Mulamwah aliweka wazi kuwa kwa sasa hachumbiani na mtu yeyote.

"Sana!" alisema.

Mwanadada mmoja kutoka nyumbani kwao Kitale alichukua hatua ya ujasiri na kumwomba mchekeshaji huyo amchukue kama mchumba wake kwa kuwa kwa sasa hayuko kwenye mahusiano yoyote.

"Niko hapa Mulamwah.. Natraka kuwa mchumba wako, Msichana wa Kiluhya kutoka Kitale," aliandika mwanadada huyo.

Mulamwah alimjibu, "Unarisk!"

Mpenzi huyo wa zamani wa muigizaji Carrol Sonnie pia alionekana kupuuza maombi mengi ya kukutana kutoka kwa mashabiki wake.

Kando na kuweka wazi kuwa hayupo kwenye mahusiano yoyote kwa sasa, Mchekeshaji huyo pia alibainisha kuwa muda mrefu umepita sasa tangu aliposhiriki tendo la ndoa kwa mara ya mwisho.

Mulamwah na Carrol Sonnie walitangaza kutengana kwao mwaka jana, takriban miezi miwili tu baada ya kukaribisha mtoto wao wa kwanza pamoja.

"Hii ni kuweka wazi kuwa mimi na Mulamwah hatuko pamoja tena. Sote wawili tumekubali kuachana kwa sababu zinazojulikana kwetu. Asanteni sana kwa upendo na sapoti mliyotupa kwa miaka hiyo minne, binafsi siichukulii hivihivi," Sonnie alisema kupitia mitandao ya kijamii mnamo Disemba 2021.

Kwa upande wake, Mulamwah alibainisha kuwa uamuzi wa kutengana na mama huyo wa binti haukuwa rahisi kamwe.

"Huu haukuwa uamuzi rahisi kufanya, haswa katika wakati huu wa maisha yangu. Umekuwa mwaka mgumu kwangu, na kwa sisi sote pia, karibu kupoteza kila kitu. Haya yote yanayotokea sasa yameunganishwa na kuongezwa na 'anthology' ya hivi majuzi ya matukio yanayojulikana zaidi kwetu," alisema.

Matukio yaliyofuatia utengano huo na yanayoendelea kujitokeza yalifichua kuwa uhusiano kati ya wawili hao sio mzuri. 

Haijulikani wazi ikiwa wapenzi hao wa zamani wanashirikiana katika malezi ila Mulamwah amekuwa akidai kuwa amenyimwa nafasi ya kuwa katika maisha ya bintiye wala kumuona.