Wanawe Zari wamlaumu kwa kusambaratika kwa familia yake na Diamond

"Lakini sasa yuko na mtu mwingine, nasema ukweli," Tiffah alimwambia Diamond.

Muhtasari

•Ndugu hao wawili wanaoishi na Zari nchini Afrika Kusini pia hawaamini kuwa baba yao ana watoto wengine mbali na wao.

•Tiffah alimlamikia mama yake kwa kuvunja familia huku akimkosoa kwa kujitosa kwenye mahusiano na mwanaume mwingine.

Diamond Platnumz, Prince Nillan, Tiffah Dangote na Zari Hassan
Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Tiffah Dangote na Prince Nillan wanaamini kuwa baba yao Diamond Platnumz hakusababisha kusambaratika kwa mahusiano yake na mama yao, Zari Hassan.

Ndugu hao wawili wanaoishi na Zari nchini Afrika Kusini pia hawaamini kuwa baba yao ana watoto wengine mbali na wao.

Wakati wa kikao cha familia ambacho waliitisha wakati staa huyo wa Bongo alipowatembelea jijini Johanesburg, ndugu hao wawili walimlaumu mama yao kwa kutengana kwa yao familia miaka kadhaa iliyopita.

"Lakini sasa yuko na mtu mwingine, nasema  ukweli," Tiffah alimwambia Diamond.

Mwimbaji huyo ambaye awali katika kikao hicho alikuwa amewahakikishia watoto wake kuhusu mapenzi yake makubwa kwa mama yao alijifanya kushtuka sana kusikia kuwa mzazi huyo mwenzake anachumbiana na mwanaume mwingine.

Prince Nillan aliyaunga mkono madai ya dadake dhidi ya mama yao na kuonekana kuuegemea zaidi upande wa baba yake Diamond.

"Kwa hiyo ni Mama T aliyevunja familia!" aliongeza Nillan.

Ndugu hao wawili wenye umri wa miaka 7 na 5 pia walikanusha madai kuwa baba yao yuko katika mahusiano na mwanamke mwingine.

"Siamini una mpenzi mwingine siamini una watoto wengine," alisema Tiffah.

Zari ambaye alikuwa akifuatilia kwa makini wakati watoto wake wakiibua madai mazito mazito dhidi yake alionekana kushangazwa sana na jinsi walivyogeuza kidole cha lawana kutoka kwa mpenzi huyo wake wa zamani na kuelekeza kwake.

Tiffah aliendelea kumlalamikia mama yake kwa kuvunja familia huku akimkosoa kwa kujitosa kwenye mahusiano na mwanaume mwingine.

"Kwa nini uliivunja familia? Uko na mtu mwingine, unatumia muda wako naye, huna wakati na familia, hatumii wakati wako na baba!" alimlalamikia mamake.

Alilalamika sana kuhusu hatua ya mamake kutumia muda mwingi na mpenzi wake mpya siku za wikendi badala ya kuwa na baba yao Diamond.

"Ondoka hapa, ulivunja familia" alimwambia.

Licha ya kufurahishwa na wanawe kwa kutomshtumu kwa kusababisha kuvunjika kwa familia, Diamond hata hivyo alimtetea mpenzi huyo wake wa zamani kwa watoto wao na kuwahakikishia kuwa familia bado ipo imara.

"Hatukuvunja familia. Familia bado iko imara," aliwaambia.

 Aliongeza "Mkimuona na mtu mwingine anaigiza tu. Kama vile tu huwa mnaona nikifanya katika video za muziki."