Sitetei jinsia yoyote - Nameless ajivunia kuwa baba wa mabinti watatu

Nameless alisema suala la kuzingatia jinsia ya kiume ni mambo ya kizamani.

Muhtasari

• Nameless alimpokea binti yake wa tatu hivi majuzi, suala ambalo shabiki wake mmoja alitoa maoni yake na kumwambia atafute mtoto wa kiume

• Mwanamuziki huyo amechukulia suala hilo kama suala la kizamani.

Nameless na Shiru

Mwanamuziki Nameless amezungumzia suala la kijinsia na kusema kuwa yeye hatetei jinsia yoyote.

Nameless alisema kuwa yeye kibinafsi ni mtu atakayetetea jinsia yoyote ile hata kuwe na jambo gani.

Aliongeza kuwa habagui jinsia yoyote na atapenda mtoto yeyote awe wa kike au wa kiume na sio kulingana na mila.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa wanamila au wazee wa kitambo ndio waliokuwa wakibagua jinsia na hata kutetea jinsia moja kuliko nyingine.

"Kama unanijua vizuri, unajua kuwa nitapigania mtoto wa kike na pia nitapigania mtoto wa kiume. Sina ubaguzi. Sina uaminifu kwa pande moja tu, nina uaminifu kwa matendo ya haki," Nameless alifafanua maoni yake.

Mume huyo wa Wahu alisema kuwa bado ataendelea kuwa baba ya mabinti watatu hata watu waseme nini.

Alisema kuwa atamtetea bintiye na kuendelea na jukumu lake la kuwalea mabinti wake kama inavyostahili.

Aliwahimiza watu kuepuka mila na desturi ya kuona  jinsia moja ambayo ni ya kiume kuwa jinsia inalostahili sana katika familia.

Hii ni baada ya shabiki wake mmoja, siku mbili zilizopita, kujibu kwenye picha aliyokuwa amepakia Nameless katika ukurasa wake wa Facebook.

Shabiki huyo alimwambia Nameless atafute mtoto wa kiume kwa sababu ya mila na desturi za kiafrika zinazoangazia jinsia hiyo kwa sana.

"Tafuta kijana boss, jina lako, sisi ni Waafrika," Dalphine Memba alimwambia mwanamuziki huyo.

Wakati huo huo, Nameless alimjibu shabiki huyo na kumkosoa kwa anavyofikiria na kumwambia kuwa yeye yuko sawa na kulea mabinti wake watatu.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa watu wanafaa kuwa na hekima wakitaka kuangazia suala hilo la kijinsia.

Alisema kuwa alielewa kuwa watu wamefunzwa kuangazia sheria za kimila zinazohusu jinsia ila sasa watu wanafaa kusonga mbele.

Aliongeza kuwa mila ni jambo ambalo linamkuza kwa uongozi na kuwa mila ambazo watu wanaangazia bado ni za kitambo na zimepitwa na wakati.

"Dalphine Memba, nataka jina langu likumbukwe kama baba wa mabinti watatu ambapo wamejawa na hekima, unyenyekevu na upendo. Mabinti ambao wataishi maisha ya kuwajibika utakaompa kila mtu amani na furaha. Kwao hicho ndicho nilichopanga," Nameless alimjibu mtumizi huyo wa Facebook.