(+video) Mwanaume avua nguo benkini akiteta kupotea kwa Ksh 417k kutoka kwa akaunti yake

Mwanaume huyo alieleza kuwa zaidi ya laki nne hizo zilitoweka kwa njia za utatanishi kutoka kwa akaunti yake.

Muhtasari

• Wengi wa watumizi wa mitandao walimuunga mkono kwa kusema kwamba uchumi umedorora na pesa za mtu kupotea kwa njia tatanishi si kitu cha kufurahisha.

Bila shaka ni kweli kwamba mfumuko wa kiuchumi unazidi kukata zaidi katika maisha ya watu wenye kipato cha kadri katika mataifa mengi ya bara la Afrika.

Athari hizi za kiuchumi zinafanya mtu kuthamini hata senti moja iliyoko kwenye akaunti yake na si jambo la masihara kuona pesa zako zinatoweka katika mazingira ya kutatanisha, haswa zikiwa kwenye akaunti yako ya benki ambapo usalama wa fedha ni hakikisho tosha.

Sasa kuna video moja ambayo imekuwa ikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha mwanaume mmoja akizua varangati kwenye benki baada ya kugundua kwamba maelfu ya pesa zake zimepotea kwa njia ya kutatanisha kutoka kwa akaunti yake.

Katika video hiyo ambayo ilipakiwa na blogu moja, mtu mchapakazi mwenye umri wa kati ya miaka 30 hadi 40 alikwenda kwenye moja ya benki za Lagos kudai kuwa kiasi cha Naira milioni 1.5 ambazo ni sawa na shilingi 417,943 pesa za Kenya.

Mwanaume huyo alizua kioja kwenye benki hiyo baada ya kugundua pesa hizo zilitoweka kutoka kwa akaunti yake pasi na yeye kufahamishwa, na picha lilianza akijibwaga chini na kuanza kuvua shati huku akiteta.

Wafanyakazi na wateja wengine waliokuwepo walimsihi kuwa na subira kwa sababu kila kitu kitakuwa sawa kwa wakati wake. Wafanyakazi hao pia wanashauku ya kutaka kujua ni nini kilisababisha upotevu wa ghafla wa fedha kwenye akaunti yake, hivyo afisa wa usalama hakujaribu hata kutumia nguvu kumwondoa kwa sababu kila mtu aliamini anafanya hivyo kudai haki.

Dakika chache baada ya video hii kupakiwa mtandaoni, kulikuwa na maoni tofauti kutoka kwa Watumizi wa mtandao wa Instagram huku kila mmoja akiendelea kumimina yaliyo moyoni mwake katika sehemu ya maoni ya chapisho lililo na maelezo ya video hiyo.

“Milioni zote 1.5 nzima na mwanamume huyu bado anashughulikia hali hiyo akiwa na glavu za watoto ... kama 1500 zimekosa kwa akaunti yangu na mimi kuchukua hii miguu yangu miwili kuingia benki .... kuna vita ya dunia ya 3 itaanza ....mimi nitailenga benki hii kwa kukatisha tamaa maisha yangu,” mmoja alisema.

“Yaani bado hajavua suruali, mimi sasa hivi ningekuwa nimebaki na chupi peke yangu, milioni 1.5 kupotea kwa ugumu huu wa maisha ni msala mkubwa,” Official Leczy aliongezea.