Diana Marua hospitalini tayari kujifungua mtoto wake wa tatu

Ni wazi kuwa mkewe Bahati anahesabu masaa machache tu kabla ya kujifungua.

Muhtasari

•Katika picha, Diana alionekana mwenye bashasha, mwenye hamu na tayari kupokea mzaliwa wake wa tatu.

•Takriban wiki mbili zilizopita wanandoa hao walithibitisha kuwa wanatarajia mtoto wa kike.

akiwa hospitalini tayari kujifungua mtoto wake wa tatu.
Mwanavlogu Diana Marua akiwa hospitalini tayari kujifungua mtoto wake wa tatu.
Image: INSTAGRAM// BAHATI

Ni wazi sasa kwamba wakati wa kujifungua wa mwanavlogu mashuhuri Diana Marua hatimaye umekaribia.

Diana na mume wake Bahati wanatarajia mtoto wao wa tatu pamoja.

Jumatatu jioni wanandoa hao walichapisha picha za Diana akiwa hospitalini na kudokeza kwamba anahesabu masaa machache tu kabla ya kujifungua.

"Kisia nini?? @Diana_Marua @KomarockModern," Bahati aliandika chini ya picha ya Diana akiwa amesimama kando ya gari la wagonjwa.

Katika picha, Diana alionekana mwenye bashasha, mwenye hamu na tayari kupokea mzaliwa wake wa tatu.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Diana alitangaza kuwa hospitali hiyo ni makazi yake mapya kwa muda.

"Nyumbani mbali na nyumbani," aliandika chini ya video zilizomuonyesha akitembea kwenye korido za hospitali hiyo.

Mama huyo wa watoto wawili alionyesha tumbo lake kubwa kwa fahari na hakuonyesha dalili za wasiwasi juu ya hatua iliyo mbele yake.

Mapema mwezi huu Diana na Bahati walidokeza kuwa mtoto wao wa tatu huenda akazaliwa muda wowote hivi karibuni.

Takriban wiki tatu zilizopita Bahati alitangaza kuwa ujauzito wa mkewe ulikuwa katika kipindi cha mwisho.

Msanii huyo alitoa tangazo hilo alipokuwa akiwahutubia mashabiki  wake katika tamasha la Wamusyi Night.

"Diana anatarajia kujifungua dakika yoyote sasa!" Baba huyo wa watoto watatu alisema.

Alibainisha kwamba amekuwa akikaa karibu na mkewe mara nyingi kwa sababu anaweza kupata uchungu wa leba wakati wowote.

"Lazima nikae karibu na nyumbani," alisema.

Diana kwa upande wake alidokeza kuwa safari ya ujauzito huo wake wa tatu haijakuwa rahisi na amepitia changamoto chungu nzima.

"Kuna wakati kuamka kitandani haikuwa kazi ngumu, niliweza kulala kwa nafasi yoyote, nakosa kulala juu ya tumbo langu.

Kuna wakati niliweza kutoshea saizi ya kiatu changu bila shida yoyote. Miguu yangu sasa inashindana na ile ya tembo," alisema.

Pia alibainisha kuwa hajaweza kukaa bafuni  na kuoga kwa muda mrefu kwa sababu hataki tena maji ya moto.

Takriban wiki mbili zilizopita wanandoa hao walithibitisha kuwa wanatarajia mtoto wa kike.