King Alami alijirusha kwa sababu yangu - Noti Flow ajihisi mwenye hatia

Rapa huyo alijuta baada ya aliyekuwa mpenziwe King Alami kujirusha kutoka kwenye ghorofa .

Muhtasari

• Rapa huyo alieleza jinsi alivyo tayari kupitia chochote kile na mpenzi wake na kumwombea afya njema.

• Noti flow alikiri kuwa mwenye hatia baada ya wanamitandao kumlaumu kwa kisa hicho kutendeka.

Noti Flow na King Alami

Mwanamuziki Noti Flow amewajibu waliomlaumu kwa kisa cha aliyekuwa mpenzi wake King Alami kujirusha kutoka kwa ghorofa na kueleza jinsi anavyojihisi kuwa na hatia.

Kupitia Instagram, rapa huyo alieleza jinsi alivyo tayari kupitia chochote kile na mpenzi wake na kumwombea afya njema.

"Tutakuombea mpenzi wangu, tumekuwa tukikuombea usiku na mchana. Una nguvu ya kustahimili na wewe ndiye msagaji pekee niliyezama kwenye mapenzi naye. Nakupenda sana kila siku, hakuna kilichobadilika. Niko hapa nawe milele mpenzi wangu. Pona haraka , unapendwa sana," Noti Flow aliandika.

Pia alichukua fursa kuwajibu wakosoaji waliomlaumu kwa yaliyomtendekea mpenzi wake.

"Kwa wale mnaonilaumu, asanteni kwa kufanya nihisi vibaya zaidi ya ninavyohisi na mwenye hatia ila hamjakosea, alijirusha kwa sababu yangu na kama ningekuwa naye angekuwa sawa kama alivyokuwa, mnisulubishe basi," aliandika.

Pia alichapisha picha ya kumbukumbu zake na mpenziwe kwenye Instastori zake. Picha hiyo ilionyesha kumbukumbu ya wakati ambao mapenzi yao yalikuwa yamenoga na walikuwa na mahaba mno.

Aliambatanisha picha hiyo na ujumbe mtamu wa kihisia kwa mpenziwe ambao uliwagusa wanamitandao wengi.

"Hata kifanyike nini, hata iwe siku gani, hata sababu iwe ipi, Nitakupenda kila saa na kila siku, hadi milele, " aliandika.

Hata hivyo, Noti Flow alionekana kukosa matumaini ya mahusiano yao kufufuka kama yalivyokuwa kitambo.

Alieleza jinsi anaweza kufanya jambo lolote lile hata liwe kubwa kiasi gani ili kuwa na mpenzi wake King Alami.

Alimkumbusha Alami kuwa ana uwezo wa kupambana na kuwa sawa katika hali yoyote ile.

Mpenzi huyo wa Noti Flow amelazwa hospitalini na rapa huyo amekuwa akisaidia familia yake kugharamia matibabu.

Noti Flow pia aliwaomba mashabiki wake kusaidia kulipia matibabu ili kuzuia kuwa na deni Alami atakapopata nafuu.