Msichana achoma cheti chake cha digrii kwa kukosa kazi miaka 4 tangu kuhitimu

Mwanadada huyu alichoma cheti hicho alipokosa kupata kazi miaka minne baada ya kuhitimu.

Muhtasari

• Bridget Thapwile Soko alisomea shahada ya Biashara.

• Alisema ni bora aichome shahada hiyo na kuweka cheti cha ndoa yake.

Mwanamke mmoja msomi nchini Malawi aliwaacha watu wengi wakimzungumzia baada yake kuteketeza cheti cha kuhitimu kwa madai anayosema kuwa haikumsaidia na kitu chochote.

Msichana huyu anayejulikana kama Bridget Thapwile Soko alisomea shahada ya Biashara.

Anadai alichanganyikiwa alipokosa kupata kazi miaka minne baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Exploits lililoko Malawi. 

Katika video iliyosambaa kwenye mtandao wa TikTok, mwanadada huyo aliimba na kumdhihaki kila mtu ambaye alishindwa kumtolea nafasi za kazi au hata kumwalika kumhoji kuhusu kazi.

Alisema ni bora aichome shahada hiyo na kuweka cheti cha ndoa yake.

Sauti za watu walioshuhudia tukio hilo mwanamke akichoma cheti zilisikika wakishtuka na kujaribu kumshauri aghairi hatua yake ila hakuambilika wala kusemezeka.

Usimamizi wa chuo kikuu cha Exploits ulilaani kitendo chake pindi tu walipoona video hiyo huku wakisema kitendo hicho ni kama cha kudhihaki shule hiyo.

“Kulingana na tunavyojijazia, msichana huyo alifanya hivi ili kukidhihaki chuo cha Exploits na kuchafua sifa ya chuo kikuu.''

“Kwa hivyo chuo kikuu kinabatilisha shahada ya usimamizi wa biashara uliyopewa. Msimamizi wa shule hiyo alisema.

"Kwa hivyo, wewe si mhitimu tena wa Chuo Kikuu cha Exploits na kwa hivyo cheti chako cha digrii kimebatilishwa mara moja."kauli ilitolewa na Desmond Bikoko ambaye ndiye msimamizi wa shule hiyo.

Kulingana na watumizi wa mitandao walionesha kumkashifu msichana huyo wakisema kitendo chake hakikuwa chenye busara hata kama kazi iliwa nadra sana kupatikana.